• HABARI MPYA

  Monday, March 18, 2019

  AZAM FC YAWEKA MALENGO YA KUFANYA VYEMA AZAM SPORTS FEDERATION CUP

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, siku 12 zijazo kitakuwa na mchezo muhimu wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azan Sports Federation Cup) dhidi ya Kagera Sugar utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera Machi 29 mwaka huu.
  Kwa kutambua umuhimu wa mechi za Kombe la FA, benchi la ufundi la timu hiyo limeweka wazi kuwa watacheza kama fainali mechi zote za michuano hiyo ili kutimiza adhma ya kufika fainali na kutwaa taji hilo na kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
  “Mechi za FA ni fainali kwetu, tunazichukulia kwa uzito mkubwa, nashukuru wachezaji wako vizuri kila mmoja anajitahidi kuonyesha uwezo wake kila anapopata nafasi kwenye mechi, kwa sasa siwezi nikaweka wazi tumejiandaaje kucheza na Kagera, nawasubiria wachezaji mazoezini Jumanne na kuanza mikakati ya kuwakabili,” alisema Kocha wa muda wa timu hiyo, Idd Nassor Cheche.
  Mara baada ya kuichapa Singida United mabao 4-0 kwenye mchezo wa uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), wachezaji wa Azam FC wanatarajia kurejea mazoezini keshokutwa Jumanne tayari kuanza maandalizi ya mchezo huo.
  Wachezaji wote wanatarajia kurejea mazoezini Jumanne, isipokuwa nyota wanne wa kikosi hicho walioitwa timu za Taifa, ambao ni Nahodha Agrey Moris, kiungo Mudathir Yahya (Tanzania), Nickolas Wadada (Uganda) na Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe).
  Kikosi hicho kinatarajia kuanza safari ya kuelekea mkoani Kagera, Machi 25 alfajiri, ikiwa ni safari ya siku mbili, ikitarajia kuwasili mjini Bukoba siku inayofuata tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.
  Azam FC ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Rhino Rangers mabao 3-0, yaliyofungwa na viungo washambuliaji Tafadzwa Kutinyu, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji Obrey Chirwa.
  Kagera Sugar yenyewe iliichapa Boma FC ya mkoani Mbeya mabao 2-1, mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba huku wenyeji hao wakitoka nyuma na kupata ushindi huo.
  Msimu huu kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi, Novemba mwaka jana Azam FC ilikipiga na Kagera Sugar katika dimba hilo na kupata ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Donald Ngoma, akiunganisha pasi ya Kutinyu.
  Wanafainali hao wa michuano hiyo msimu 2015/2016, wakifika hatua hiyo na kupoteza dhidi ya Yanga (3-1), wamekuwa na mwenendo mzuri kwenye mechi nne zilizopita za mashindano yote baada ya kikosi kukabidhiwa kwa makocha wa muda, Idd Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, wakishinda zote.
  Walianza kuishushia kipiga Rhino Rangers, kabla ya kushinda mechi tatu mfululizo za ligi, dhidi ya African Lyon (3-1), JKT Tanzania (6-1) na Singida United (4-0), katika mechi zote hizo nne ikiwa imefunga jumla ya mabao 16, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWEKA MALENGO YA KUFANYA VYEMA AZAM SPORTS FEDERATION CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top