• HABARI MPYA

  Sunday, March 17, 2019

  HII NDIYO SIRI YA MAFANIKIO YA SIMBA SC LIGI YA MABINGWA AFRIKA

  SIMBA SC imekamilisha mechi zake za Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) usiku wa jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, Simba imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo kama mshindi wa pili wa kundi hilo kwa pointi zake tisa, nyuma ya Al Ahly ya Misri iliyoongoza kwa pointi moja zaidi baada ya mechi tano.
  JS Saoura ya Algeria, timu nyingine katika kundi hilo imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake nane, wakati AS Vita iliyomaliza na pointi saba imeshika mkia.
  Shujaa wa Simba SC jana alikuwa ni kiungo Mzambia, Clatous Chama aliyefunga bao la ushindi dakika ya 90 akimalizia pasi ya Nahodha, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco aliyesogeza krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima.

  Na hiyo ilifuatia AS Vita kutangulia kwa bao la Francis Kazadi Kasengu dakika ya 12 akimalizia mpira uliozuiwa na beki Muivory Coast wa Simba SC, Serge Wawa Pascal baada ya shuti la Fabrice Ngoma.
  Ikawachukua dakika 24 Simba SC kusawazisha bao hilo kupitia kwa beki wake wa kushoto na Nahodha Msaidizi wa klabu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyewazidi mbio mabeki wa AS Vita dakika ya 36 baada ya kutanguliziwa pasi na kiungo Muzamil Yassin.
  Mchezo mwingine wa Kundi D, Al Ahly iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura mabao ya Fateh Talah aliyejifunga dakika ya 30, Marwan Mohsen dakika ya 45 na ushei na Hussein El Shahat dakika ya 81 mjini Alexandria, Misri.
  Safari ya Simba SC katika michuano ya mwaka huu ilianzia nyumbani Januari 12, mwaka huu ikishinda 3-0 dhidi ya JS Saoura Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi akifunga bao la kwanza dakika ya 45 na ushei akimalizia pasi ya Chama, kabla ya kumsetia Mnyarwanda, Meddie Kagere kufunga la pili na la tatu dakika za 52 na 67.
  Kutoka hapo, Simba SC ikaenda kufungwa 5-0 mara mbili mfululizo, Janauri 19 mjini Kinshasa na AS Vita na Februari 2 mjini Alexandria vipigo ambavyo vilileta dharau na kejeli za kukatisha tama.
  Lakini Wekudu wa Msimbazi wakasimama imara na kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly mjini Dar es Salaam 1-0 Februari 12, bao pekee la Kagere mwenye asili ya Uganda dakika ya 65 kabla ya kwenda kuchapwa 2-0 na JS Saoura Machi 9 mjini Bechar.
  Baada ya kutimiza azma ya kushinda mechi zote za nyumbani kufuatia kuichapa na Vita jana mjini Dar es Salaam, Simba inakwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa ikiendeleza rekodi yake ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika angalau kila muongo tangu miaka ya 1970.
  Mwaka 1974 ilifika Nusu Fainali ya Klabu Afrika ikiitoa timu sumbufu ya Ghana wakati huo, Hearts Of Oak kwa kuichapa 2-1 Acrah mabao ya Abdallah KIbadeni na Adam Sabu kabla ya kutoa sare ya 0-0 Dar es Salaam.
  Lakini katika Nusu Fainali, Simba SC ikatolewa na Mehalla El Kubra kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake, ingawa kuna habari za kipa Athumani Mambosasa (sasa marehemu) kufanyiwa fujo, wakati wa upigwaji wa penalti. 
  Mafanikio makubwa miaka ya 1980 ni kufika hatua ya 16 Bora ambayo wamevuka sasa, mara mbili mwaka 1980 na 1981.
  Mwaka 1980 walitolewa na Union Douala ya Cameroon kwa jumla ya mabao 5-2, wakifungwa 4-2 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 1-0 Douala, baada ya waop kuitoa Linare ya Lesotho kwa jumla ya mabao 4-2 wakifungwa 2-l ugenini na kushinda 3-0 nyumbani na mwaka 1981 walitolewa na na JET ya Algeria baada ya kupita bila jasho Randi ya Kwanza kufuatia Horsed ya Somalia kujitoa.
  Mwaka 1993 walifika fainali ya Kombe la CAF baada ya kuzitoa Ferroviario ya Msumbiji Raundi ya Kwanza, Manzini Wanderers ya Swaziland Raundi ya Pili, USM El Harrach ya Algeria Robo Fainali, Atletico Sports Aviacao ya Angola Nusu Fainali kabla ya kufungwa na Stellah Abidjan kwenye fainali.
  Simba ililazimisha sare ya 0-0 na Stella mjini Abidjan nchini Ivory Coast Novemba 12, kabla ya kufungwa 2-0 Dar es Salaam Novemba 26 mwaka huo na kushuhudia Kombe likipandishwa ndege kuondoka nchini.
  Mwaka 2003 iliingia Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa wakati huo ikichezwa kwa mtindo wa makundi, baada ya kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamelek ya Misri katika hatua ya 16 Bora kwa penaliti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Na hiyo ni baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-1, ikishinda 1-0 Dar es Salaam na 3-0 Gaborone katika Raundi ya Awali na Santos ya Afrika Kusini kwa penalti 9-8 kufuatia sare ya jumla ya 0-0. 
  Katika Kundi A, Simba ilishinda mechi mbili nyumbani dhidi ya ASEC ya Ivory Coast 1-0 Agosti 10 na Enyimba ya Nigeria 2-1 Oktoba 5, huku mechi nyingine ikilazimishwa sare ya 0-0 na Ismailia ya Misri Septemba 7, mwaka 2003.
  Mechi za ugenini ilifungwa zote, 3-0 na Enyimba mjini Aba Agosti 10, 2-1 na Ismailia mjini Cairo Septemba 19 na 4-3 na ASEC mjini Abidjan Oktoba 19 hivyo safari yake kuishia hapo.
  Mwaka 2019, Simba tena imeendeleza rekodi yake nzuri kwenye michuano ya Afrika miongoni mwa timu za Tanzania kwa kufika Robo Fainali. 
  Siri ya mafanikio ya Simba ni malengo waliyojiwekea tangu mwanzo wanaingia kwenye mashindano ya mwaka huu, kwanza kuhakikisha lazima wanaingia hatua ya makundi.
  Na walipofuzu baada ya kuzitoa Mbabane Swallows kwa jumla ya mabao 8-1 ikishinda 4-1 Dar es Salaam na 4-0 Swaziland na Nkana FC kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 3-3, wakifungwa 2-1 mjini Kitwe na kushinda 3-1 Dar ed Salaam, wakawela malengo mapya ya kushinda mechi zote za nyumbani.
  Na kweli, wameshinda mechi zao zote za nyumbani na haijalishi walifungwa mabao 12 katika mechi tatu za ugenini, zawadi yao ni kwenda Robo Fainali wakiungana na vigogo vingine saba barani, Al Ahly, Wydad Casablanca ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Kundi B Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea, Kundi C TP Mazembe ya DRC na CS Constantine ya Algeria.
  Siri ya mafanikio ya Simba SC ni kusimamia malengo waliyojiwekea kwa gharama zozote na si kuingia kwenye mashindano kwa ajili ya kushiriki. Hongera Simba SC na kila la heri kuelekea hatua ya Nane Bora michuano ya Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HII NDIYO SIRI YA MAFANIKIO YA SIMBA SC LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top