• HABARI MPYA

  Tuesday, March 19, 2019

  MAREFA WA GABON KUCHEZESHA TAIFA STARS NA UGANDA KUFUZU AFCON JUMAPILI TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa mwisho wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu kati ya wenyeji, Tanzania na Uganda Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam utachezeshwa na marefa kutoka nchini Gabon.
  Hao ni Eric Arnaud Otogo Castane atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Moussounda Montel na Marlaise Ditsoga Boris na mchezo utaanza Saa 1:00 usiku.
  Wakati huo huo, mechi kati ya Cape Verde na Lesotho mjini Praia itachezeshwa na refa Mahamadou Keita atakayesaidiwa na washika vibendera Baba Yomboliba na Nouhoum Bamba, wote wa Mali mjini Praia.

  Eric Arnaud Otogo Castane atachezeshwa mechi kati ya Tanzania na Uganda Jumapili Uwanja wa Taifa 

  Tanzania inayofundishwa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike inahitaji ushindi Jumapili ili kuangalia uwezekano wa kufuzu AFCON ya Juni nchini Misri iwapo Lesotho itafungwa au kutoa sare na Cape Verde.
  Kikosi cha Taifa Stars kimekamilika kambini, hoteli ya Bahari Beach mjini Dar es Salaam kikiendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda ambayo tayari imekwishafuzu kama kinara wa Kundi L.
  Nahodha Mbwana Ally Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji aliwasili usiku wa jana akifuatiwa na  kiungo Farid Malik Mussa na mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wanaocheza Hispania na wote wanatarajiwa kuanza mazoezi leo jioni Uwanja wa Boko Veterani. 
  Wachezaji wengine wote wanaocheza nje, Thomas Ulimwengu wa JS Saoura ya Algeria, Himid Mao wa Petrojet, Yahya Zayd wa Ismailia, Shiza Kichuya wa ENPPI za Misri, Simon Msuva wa Difaa Jadida ya Morocco, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia wamefanya mazoezi leo asubuhi. 
  Wachezaji wazawa walipo kambini ni makipa Aishi Salum Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Metacha Mnata wa Mbao FC na Suleiman Salula wa Malindi SC.
  Mabeki ni Vincent Philipo wa Mbao FC, Ally Mtoni ‘Sonso’ wa Lipuli FC, Kennedy Wilson wa Singida United, Aggrey Morris wa Azam FC, Erasto Edward Nyoni wa Simba SC, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondan (Yanga SC). 
  Viungo ni Mudathir Yahya wa Azam FC, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na mshambuliaji John Bocco, wote wa Simba SC na mazoezi ya Taifa Stars yanatarajiwa kuhamia Uwanja wa Taifa Alhamisi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAREFA WA GABON KUCHEZESHA TAIFA STARS NA UGANDA KUFUZU AFCON JUMAPILI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top