• HABARI MPYA

  Friday, March 22, 2019

  BRUCE KANGWA AONGEZA MKATABA WA KUENDELEA KUICHEZEA AZAM FC HADI MWAKA 2021

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kushoto wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Bruce Kangwa, ameongeza mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2021.
  Awali mkataba wa beki huyo wa Kimataifa wa Zimbabwe, ulikuwa unamalizika Agosti mwaka huu, hivyo dili hilo jipya litamfanya aendelee kusalia kwenye viunga vya Azam Complex kwa miaka mingine miwili.
  Kangwa anayesifika kwa ukabaji na kasi yake kubwa ya kupandisha mashambulizi na krosi nzuri, kwa mara ya kwanza alijiunga na Azam FC mwaka Agosti 2016 akitokea Highlanders ya nchini kwao Zimbabwe.
  Bruce Kangwa (katikati) akiwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' (kulia) na Meneja, Philipo Alando (kushoto) baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili leo
  Kangwa amesaini mkataba huo leo Ijumaa mchana akiwa mbele ya Ofisa Mtendaji wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, Meneja wa timu, Phillip Alando na wakala wake, George Deda, ambao kwa pamoja walionyesha sura za furaha mara baada ya kuingia makubaliano mapya ya kuendelea kufanya kazi pamoja.
  “Nina furaha kuongeza mkataba wangu, nimefanya nao kazi tokea siku nilipofika Tanzania (mwaka 2016) ni vizuri kufanya kazi na watu wa karibu wa Azam FC na Tanzania, nafurahi kuendeleza mkataba wangu na nina matumaini kwamba nitafanya zaidi kuliko yale niliyofanya nyuma,” alisema Kangwa, alipozungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya kusaini mkataba huo.
  Kangwa anaungana na wachezaji wengine ambao tayari wameshaongeza mikataba mipya wakiwemo, beki David Mwantika, winga Joseph Mahundi na mshambuliaji Donald Ngoma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BRUCE KANGWA AONGEZA MKATABA WA KUENDELEA KUICHEZEA AZAM FC HADI MWAKA 2021 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top