• HABARI MPYA

  Monday, March 18, 2019

  SAMATTA ATOA PASI YA BAO LA TATU GENK YALAZIMISHWA SARE 3-3 UGENINI UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, WAREGEM 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana ametoa pasi ya bao la tatu timu yake, KRC Genk ikilazimishwa sare ya kufungana mabao 3-3 na wenyeji, Zulte-Waregem katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Regenboog mjini Waregem.
  Samatta alimsetia vizuri kabisa mshambuliaji mwenzake, Mbelgiji Leandro Trossard kuifungia Genk bao la tatu dakika ya 61 baada ya kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy kufunga la kwanza dakika ya 19 Mjapan na Junya Ito kufunga la pili dakika ya 39.
  Mabao ya Zulte-Waregem yalifungwa na mshambuliaji Mtunisia, Hamdi Harbaoui mawili kwa penalti dakika ya 13 na dakika ya 90 na ushei na Sandy Walsh dakika ya 72.
  Mbwana Samatta jana ametoa pasi ya bao la tatu, KRC Genk ikilazimishwa sare ya 3-3 na Zulte-Waregem
  Wakati Genk inafikisha pointi 63 baada ya kucheza mechi 30 na kuendelea kuongoza Ligi ya Ubelgiji kwa pointi saba zaidi ya Club Brugge, kwa upande wao Zulte-Waregem wanafikisha pointi 33 katika mechi ya 30, ingawa wanabaki nafasi ya 11 kwenye ligi ya timu 16.
  Harbaoui amefikisha mabao 18 sasa na kumkaribia Samatta anayeongoza kwenye chati ya wafungaji Ligi ya Ubelgiji kwa mabao yake 20.
  Samatta mwenye umri wa miaka 26, jana amecheza mechi ya 146 kwenye mashindano yote na kufunga mabao 59 tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 113 na kufunga mabao 44 na kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili na Europa League amecheza mechi 24 na kufunga mabao 14.
  Kikosi cha Zulte-Waregem kilikuwa; Bossut, De Fauw, Baudry, Harbaoui, Bongonda, De Pauw/Walsh dk45, Bjordal, Seck, Burki/Soisalo dk45, Peeters na Pletinckx/Sylla dk83.
  KRC Genk; Vukovic, Maehle, Dewaest, Lucumi, De Norre, Heynen, Malinovskyi/Ingvartsen dk85, Piotrowski/Berge dk60, Ito/Ndongala dk70, Trossard na Samatta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA ATOA PASI YA BAO LA TATU GENK YALAZIMISHWA SARE 3-3 UGENINI UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top