• HABARI MPYA

  Sunday, March 24, 2019

  TANZANIA OYEEE, TAIFA STARS YAIGONGA UGANDA 3-0 NA KUFUZU AFCON 2019

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imefuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya kiungo wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happygod Msuva na mabeki, Erasto Edward Nyoni wa Simba SC na Aggrey Morris Ambroce wa Azam FC za nyumbani, Tanzania na Uganda kufuzu kutoka Kundi L.
  Taifa Stars imefuzu kama mshindi wa pili wa kundi kwa pointi zake nane, nyuma ya Uganda iliyomaliza na pointi 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
  Wachezaji wa Taifa Stars wakifurahia baada ya bao la pili lililofungwa na Erasto Nyoni kwa penalti
  Wachezaji wa Taifa Stars wakmpongeza Erasto Nyoni baada ya kufunga bao la pili leo Uwanja wa Taifa 
  Erasto Nyoni akipiga hesabu kabla ya kuutenga mpira apige penalti  
  Nahodha Mbwana Samatta (kushoto) akimpongeza Simon Msuva baada ya kufunga bao la kwanza

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Eric Arnaud Otogo Castane aliyepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Moussounda Montel na Marlaise Ditsoga Boris wote kutoka Gabon, hadi mapumziko Taifa Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na Msuva, mchezaji wa zamani wa Yanga dakika ya 21 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji wa Simba SC ya nyumbani, John Raphael Bocco aliyeuwahi mpira uliowapita walinzi wa The Cranes kufuatia krosi ya beki wa kushoto Garidel Michael Mbaga.
  Na kipindi cha pili, Taifa Stars baada ya kuongezewa maarifa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike ikaenda kuongeza mabao mawili.
  Alianza beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Nyoni kufunga kwa penalti dakika ya 51 baada ya Kirizestom Ntambi kuunawa mpira uliopigwa na Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta, mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji.
  Akafuatia beki mwingine, Aggrey Morris kufunga kwa kichwa dakika ya 57 akimalizia krosi nzuri ya mchezaji mwenzake wa zamani wa Azam FC, Bocco kutoka upande wa kulia.    
  Uganda wakapoteana baada ya bao hilo na kuwapa nafasi Tanzania kutawala zaidi mchezo huo, lakini wakaishia kukosa tu mabao ya wazi.
  Mechi nyingine ya mwisho ya Kundi L leo, Cape Verde imelazimishwa sare ya 0-0 na Lesotho mjini Praia.
  Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kufuzu AFCON kihistoria, baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria na kwa ushindi huu, kila mchezaji atapatiwa donge nono la Sh. Milioni 10, ahadi ya Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, chini ya Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.  
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Simon Msuva/Thomas Ulimwengu dk89, Mudathir Yahya, John Bocco/Feisal Salum dk81, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Himid mao dk70.
  Uganda; Dennis Onyango, Nico Wadada, Godfrey Walusimbi, Allan Kyambadde, Moses Waiswa, Farouk Miya, Kirizestom Ntambi, Dennis Awany, Thadeo Lwanga, Emmanuel Okwi na Patrick Kaddu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TANZANIA OYEEE, TAIFA STARS YAIGONGA UGANDA 3-0 NA KUFUZU AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top