• HABARI MPYA

  Sunday, March 24, 2019

  KIUNGO WA KAGERA SUGAR, BEHEWA SEMBWANA AFARIKI DUNIA LEO DAR ES SALAAM

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO chipukizi wa klabu ya Kagera Sugar, Behewa Sembwana amefariki dunia Alfajiri ya leo mjini Dar es Salaam akiwa anakaribia kutimiza umri wa miaka 24, baada ya kusumbuliwa na maradhi ya tumbo kwa muda mrefu.
  Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amethibitisha kifo cha mchezaji huyo alipozungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Bukoba.
  Mexime amesema kwamba msiba upo nyumbani kwa mama wa marehemu, Kitunda mjini Dar es Salaam lakini marehemu anaweza kusafirishwa kwao, Tanga kwa mazishi.
  “Tunawasiliana na familia ya marehemu kujua zaidi wamepangaje, kwa sababu msiba umetokea leo, hivyo ni mapema kwetu kusema mambo mengi,”amesema Mexime.
  Behewa Sembwana amefariki dunia Alfajiri ya leo mjini Dar es Salaam akiwa anakaribia kutimiza umri wa miaka 24 

  Mexime amesema kwamba Sembwana alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya tumbo yaliyoanzia tangu anachezea Coastal Union ambako aliwahi kufanyiwa upasuaji wa utumbo na tatizo lake likajirejea akiwa Kagera Sugar ambako ilibidi afanyiwe tena upasuaji.
  “Upasuaji aliofanyiwa Hospitali ya hapa Bukoba, haukufanikiwa ikabidi ahamishiwe hospitali ya Bugando mjini Mwanza, nako pia mambo hayakwenda vizuri akahamishiwa Muhimbili mjini Dar es Salaam na huko pia mambo hayakuwa mazuri, hatimaye Mungu amemchukua kiume wake,”amesema.

  Behewa Sembwana aliondolewa kwenye kikosi cha Kagera Sugar tangu januari kutokana na matatizo ya tumbo

  Mexime alisema kwamba matatizo ya Sembwana yalianza tena akiwa Kagera Sugar katika mchezo dhidi ya Mwadui FC Jumapili ya Januari 6, mwaka huu na tangu hapo akaondolewa kwenye kikosi kwa ajili ya matibabu.
  Sembwana aliyetarajiwa kutimiza umri wa miaka 24 Aprili 5, mwaka huu pamoja na Kagera Sugar na Coastal Union, pia enzi za uhai wake aliwahi kuchezea Njombe Mji FC.  Mungu ampumzishe kwa amani Behewa Sembwana, kijana aliyekuwa anainukia vizuri kisoka nchini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIUNGO WA KAGERA SUGAR, BEHEWA SEMBWANA AFARIKI DUNIA LEO DAR ES SALAAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top