• HABARI MPYA

  Wednesday, March 27, 2019

  ABDALLAH KHERI 'SEBO' AONGEZA MKATABA WA MIAKA MITATU AZAM FC HADI 2022

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI kisiki wa kati wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Abdallah Kheri maarufu kama Sebo, ameongeza mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2022.
  Mkataba wa awali wa nyota huyo ulikuwa unamalizika Mei mwaka huu, ambapo kwa kusaini mkataba huo mpya, sasa ataendelea kubakia kwenye viunga vya Azam Complex kwa muda wa misimu mingine mitatu ijayo.
  Zoezi la kusaini mkataba huo lilifanyika jana mchana, likishuhudiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, Meneja wa timu ya vijana, Luckson Kakolaki na mmmoja wa maofisa wa timu hiyo, Abubakar Mapwisa.
  Abdallah Kheri 'Sebo' (kushoto) akisaini mkataba wa miaka mitatu kuendelea kuitumikia Azam FC hadi mwaka 2022 huku akishuhudiwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin 'Popat' 

  Nyota huyo amekuwa mhimili wa kikosi cha Azam FC msimu huu kwenye mechi za awali za ligi kabla ya kuumia, pia akiwa sehemu ya nguzo kwenye eneo la kati la ulinzi iliyowezesha mafanikio ya timu hiyo kutwaa taji la Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo Julai mwaka jana akiwa sambamba na Nahodha Agrey Moris.
  Sebo ambaye pia ni mchezaji wa timu za Taifa za Tanzania na Zanzibar, kwa sasa yupo nje ya dimba akiuguza majeraha ya goti aliyoyapata Desemba mwaka jana, yatakayomfanya kuwa nje ya dimba kwa muda wa miezi tisa hadi Agosti mwaka huu atakaporejea kwenye ushindani.
  Uongozi wa Azam FC upo kwenye mchakato wa kurefusha mikataba kwa wachezaji wote ambao mikataba yao inaelekea ukingoni, hadi sasa nyota wengine walikwishasaini mikataba mipya ni mabeki David Mwantika, Bruce Kangwa, winga Joseph Mahundi na mshambuliaji Donald Ngoma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ABDALLAH KHERI 'SEBO' AONGEZA MKATABA WA MIAKA MITATU AZAM FC HADI 2022 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top