• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 16, 2019

  NDOTO ZA UBINGWA ZAZIDI KUYEYUKA YANGA SC BAADA YA KUCHAPWA 1-0 NA LIPULI

  Na Mwandishi Wetu, IRINGA
  YANGA SC imezidi kupoteza matumaini ya ubingwa baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Lipuli FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Bao lililoizamisha Yanga limefungwa na beki Ramadhani Haruna Shamte kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita zaidi ya 20 pembezoni mwa Uwanja kushoto ambalo lilimpita kipa Klausi Kindoki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiruka kwa udhahidi.
  Kwa matokeo hayo, Lipuli FC inafikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 31 na kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu kutoka ya sita, wakati Yanga SC inayobaki na pointi zake 67katika mechi ya 28 inaendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 59 za mechi 28.

  Kwa kupoteza mechi ya tatu leo, Yanga SC inazidi kupunguza uwezekano wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kutokana na mwenendo mzuri wa mahasimu wao, Simba SC waliopo nafasi ya tatu kwa pointi zao 51 za mechi 20. 
  Baada ya kubanwa kipindi cha kwanza katika mchezo wa leo, kipindi cha pili, Yanga ambayo ilicheza bila kocha wake Mkuu, Mkongo Mwinyi Zahera ambaye amesafiri kwa majukumo ya taifa ya nchi yake, DRC ilibadili mipango ikiongeza mshambuliaji Amissi Tambwe na kutoa kiungo, Thabani Kamusoko.
  Mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mashambulizi ya Yanga kwenye lango la Lipuli, lakini bahati haikuwa yao wana Jangwani leo kwani waliishia kupoteza nafasi nzuri walizotengeneza.
  Na Lipulimiliyoongozwa na mshambuliaji mwenyen nguvu, Paul Nonga akishirikiana na chipukizi Miraj Athumani ‘Madenge’ iliendelea kulitia misukosuko lango la Yanga kwa mashambulizi ya kushitukiza.
  Mshambuliaji Heritier Makambo kutoka DRC leo hakuwa katika ubora wake kutokana na kupoteza nafasi nyingi, huku Tambwe naye akidhibitiwa vizuri baada ya kuingia.  
  Kiungo Deus David Kaseke ni mchezaji mwingine wa Yanga ambaye hakuwa na bahati leo kutokana na kupoteza nafasi nyingi, ikiwemo ya dakika ya 58 shuti lake dhaifu lilipookolewa na kipa Yusuph Mohammed ndani ya boksi.
  Kikosi cha Lipuli FC kilikuwa; Yusuph Mohammed, Haruna Shamte, Paul Ngalema, William Lucian ‘Gallas’, Novaty Lufunga, Freddy Tangalu, Zawadi Mauya/Issa Mgoha dk80, Jimmy Shoji, Paul Nonga, Daruesh Saliboko/Steven Sylvester dk33 na Miraj Athumani ‘Madenge’/Ally Sonso dk89.
  Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael/Haruna Moshi ‘Boban’ dk85, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondan, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngassa, Thabani Kamusoko/Amissi Tambwe dk54, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Deus Kaseke/Jaffar Mohammed dk82. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Kagera Sugar imeichaoa 2-1 Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mabao ya wenyeji yakifungwa na Ramadhan Kapera kwa penalti dakika ya 55 na Ally Ramadhani dakika ya 60 baada ya wageni kutangulia kwa bao la Jaffary Salum Kibaya dakika ya saba, huku Coastal Union ikilazimishwa sare ya 0-0 na Alliance FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Mabao ya Eric Kyaruzi dakika ya 56 na Hamidu Mohamed dakika ya 67 yakaipa ushindi wa 2-0 Mbeya City dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wakati bao pekee la Daniel Manyenye dakika ya 15 likaipa ushindi wa 1-0 Biashara United dhidi ya African Lyon Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NDOTO ZA UBINGWA ZAZIDI KUYEYUKA YANGA SC BAADA YA KUCHAPWA 1-0 NA LIPULI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top