• HABARI MPYA

    Thursday, March 21, 2019

    WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI MECHI YA TAIFA STARS NA UGANDA JUMAPILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa mwisho wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu kati ya wenyeji, Tanzania na Uganda Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Saida Taifa Stars Ishinde, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba Waziri Mkuu, Majaliwa amekubali wito wa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo.
    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa kutoka nchini Gabon ambao ni Eric Arnaud Otogo Castane atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Moussounda Montel na Marlaise Ditsoga Boris na mchezo utaanza Saa 1:00 usiku.
    Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika mchezo kati ya Tanzania na Uganda Jumapili Uwanja wa Taifa 

    Mechi kati ya Cape Verde na Lesotho mjini Praia itachezeshwa na refa Mahamadou Keita atakayesaidiwa na washika vibendera Baba Yomboliba na Nouhoum Bamba, wote wa Mali mjini Praia.
    Tanzania inayofundishwa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike inahitaji ushindi Jumapili ili kuangalia uwezekano wa kufuzu AFCON ya Juni nchini Misri iwapo Lesotho itafungwa au kutoa sare na Cape Verde.
    Kikosi cha Taifa Stars kimekamilika kambini, hoteli ya Bahari Beach mjini Dar es Salaam kikiendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda ambayo tayari imekwishafuzu kama kinara wa Kundi L.
    Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na wengine wanaocheza nje, kiungo Farid Malik Mussa na mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wanaocheza Hispania, Thomas Ulimwengu wa JS Saoura ya Algeria, Himid Mao wa Petrojet, Yahya Zayd wa Ismailia, Shiza Kichuya wa ENPPI za Misri, Simon Msuva wa Difaa Jadida ya Morocco, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia wote wapo vizuri. 
    Wachezaji wazawa walipo kambini ni makipa Aishi Salum Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Metacha Mnata wa Mbao FC na Suleiman Salula wa Malindi SC.
    Mabeki ni Vincent Philipo wa Mbao FC, Ally Mtoni ‘Sonso’ wa Lipuli FC, Kennedy Wilson wa Singida United, Aggrey Morris wa Azam FC, Erasto Edward Nyoni wa Simba SC, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondan (Yanga SC). 
    Viungo ni Mudathir Yahya wa Azam FC, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na mshambuliaji John Bocco, wote wa Simba SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI MECHI YA TAIFA STARS NA UGANDA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top