• HABARI MPYA

  Wednesday, March 20, 2019

  SIMBA SC KUMENYANA NA TP MAZEMBE ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA, ITAANZIA NYUMBANI

  Na Mwandishi Wetu, CAIRO
  SIMBA SC itamenyana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwezi ujao.
  Katika droo iliyopangwa leo ukumbi wa Aida Ballroom, Marriot Zamalek mjini Cairo, Misri, washindi wa kwanza wa Kundi D, Al Ahly ya Misri watamenyana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, CS Constantine ya Algeria itamenyana na Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea na Wydad Casablanca ya Morocco.
  Simba SC ambayo iliwakilishwa na Mwenyekiti, Swedi Nkwabi na Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori Katika droo hiyo, itaanzia nyumbani kati ya Aprili 5 na 6 kabla ya kusafiri kwenda Lubumbashi kwa mchezo wa marudiano Aprili 12 au 13.

  Ikifanikiwa kuingia Nusu Fainali itamenyana na mshindi kati ya CS Constantine na Esperance, wakati Al-Ahly ikifuzu itamenyana na mshindi kati ya Horoya Guinea na Wydad Casablanca mechi za kwanza zikichezwa kati ya Aprili 26 na 27 na marudiano Mei 3 na 4, mwaka huu.
  Fainali ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019 itafanyika Mei 24 na marudiano Mei 31 na ikumbukwe bingwa mtetezi ni Esperance waliomfunga Al Ahly mwaka jana. 
  Simba SC imefika hatua hii baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D kwa pointi zake tisa, nyuma ya Al Ahly iliyomaliza na pointi 10 na mbele ya JS Saoura ya Algeria iliyomaliza na point inane na AS Vita ya DRC iliyomaliaa na pointi saba.
  Awali ya hapo Simba SC iliitoa Mbabane Swallows kwa jumla ya mabao 8-1 ikishinda 4-1 Dar es Salaam na 4-0 Swaziland, kabla ya kwenda kuitoa na Nkana FC kwa jumla ya mabao 4-3, ikifungwa 2-1 Kitwe na kushinda 3-1 Tanzania.
  Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, timu ya Nkana FC ya Zambia yenye beki Mtanzania, Hassan Ramadhani Kessy itamenyana na CS Sfaxien ya Tunisia wakianzia nyumbani Aprili 7 kabla ya kwenda Tunis Aprili 14.
  Etoile du Sahel ya Tunisia itamenyana na Al-Hilal ya Sudan, Hassania Agadir na Zamalek ya Misri, Gor Mahia ya Kenya na RS Berkane ya Morocco.
  Ikienda Nusu Fainali Nkana FC itamenyana na mshindi kati ya Gor Mahia na RS Berkane, wakati mshindi kati ya Etoile du Sahel na Al-Hilal atamenyana na mshindi kati ya Hassania Agadir na Zamalek, mechi za kwanza zikichezwa Aprili 28 na marudiano Mei 5.
  Fainali ya kwanza ya Kombe la Kombe la Shirikisho msimu wa 2018-2019 itachezwa Mei 19 na marudiano yatakuwa Mei 26.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUMENYANA NA TP MAZEMBE ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA, ITAANZIA NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top