• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 17, 2019

  NDANDA FC YAICHAPA KMC 2-0 LIGI KUU UWANJA WA NANGWANDA SIJAONA

  Na Mwandishi Wetu, MTWARA
  TIMU ya Ndanda FC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
  Ushindi huo wa Ndanda FC katika Uwanja wa nyumbani, umetokana na mabao ya Carlos Kirenge aliyejifunga dakika ya 52 na Yusuph Mhilu dakika ya 56.
  Na kwa ushindi huo, Ndanda FC inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 29 na kujiinua kidogo kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya timu 20 hadi nafasi ya 15 kutoka ya 18, wakati KMC inayobaki na pointi zake 41 baada ya kucheza mechi 30, inabaki nafasi ya tano.

  Mechi za Ligi Kuu jana, Yanga SC ilizidi kupoteza matumaini ya ubingwa baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Lipuli FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Bao lililoizamisha Yanga lilifungwa na beki Ramadhani Haruna Shamte kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita zaidi ya 20 pembezoni mwa Uwanja kushoto ambalo lilimpita kipa Klausi Kindoki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiruka kwa udhahidi.
  Kwa matokeo hayo, Lipuli FC imefikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 31 na kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu kutoka ya sita, wakati Yanga SC inayobaki na pointi zake 67katika mechi ya 28 inaendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 59 za mechi 28.
  Nayo Kagera Sugar iliichapa 2-1 Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mabao ya wenyeji yakifungwa na Ramadhan Kapera kwa penalti dakika ya 55 na Ally Ramadhani dakika ya 60 baada ya wageni kutangulia kwa bao la Jaffary Salum Kibaya dakika ya saba, huku Coastal Union ikilazimishwa sare ya 0-0 na Alliance FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Mabao ya Eric Kyaruzi dakika ya 56 na Hamidu Mohamed dakika ya 67 yakaipa ushindi wa 2-0 Mbeya City dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wakati bao pekee la Daniel Manyenye dakika ya 15 likaipa ushindi wa 1-0 Biashara United dhidi ya African Lyon Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NDANDA FC YAICHAPA KMC 2-0 LIGI KUU UWANJA WA NANGWANDA SIJAONA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top