• HABARI MPYA

  Wednesday, March 27, 2019

  RAIS WA TFF WALLACE KARIA AWASHUKURU WATANZANIA KUIUNGA MKONO TAIFA STARS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Wallace Karia ametoa shukrani za dhati kwa Serikali, Taasisi Mbalimbali, Vyombo vya Habari, Vyombo vya Usalama na kila Mtanzania kwa kuiunga mkono Timu ya Taifa “Taifa Stars”.
  Amesema TFF inaamini kila mmoja alihamasika kuiunga mkono Taifa Stars hasa kutokana na kiu ya kila mmoja kuona  inacheza AFCON.
  “Hakika ilikuwa hamasa kubwa na Uzalendo wa hali ya juu ambao unapaswa kupongezwa kwa namna ambavyo kila mmoja alijitoa kwa nafasi yake kwaajili ya timu yake ya Taifa” Amesema Rais wa TFF Ndugu Karia.
  Uungwaji mkono uliofanyika kwa Taifa Stars ni sehemu kubwa ya morali kwa wachezaji na TFF inaamini Watanzania wataendelea kuziunga mkono timu za Taifa na Wawakilishi wa Tanzania wanaokabiliwa na mashindano ya Kimataifa.

  Rais wa TFF, Wallace Karia ameishuku Serikali na Taasisi Mbalimbali kwa kuiunga mkono Taifa Stars 

  Kwa sasa timu ya Taifa ya Wanawake “Twiga Stars” ipo Kambini ikijiandaa na mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu Olympic dhidi ya DR Congo utakaochezwa April 5,2019,Pia timu ya Vijana U17 “Serengeti Boys” ipo Kambini ikijiandaa na mashindano ya AFCON ya Vijana U17 yatakayofanyika Tanzania April 14-28,2019.
  Karia amewaomba Watanzania waziunge mkono timu hizo kwa kujitokeza kwa wingi ili kuwa sehemu ya hamasa ya kufanya vizuri kwa timu zetu.
  TFF itaendelea kuhakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ili kupata matokeo chanya katika mashindano yanayowakabili.
  Ni Imani ya TFF kuwa Watanzania wataendelea kujitokeza kwa wingi Uwanjani kuziunga mkono timu zetu kama ilivyokua kwa Taifa Stars.
  Vyombo vya Habari ambao ni moja ya Wadau wakubwa tunaamini tutaendelea kushirikiana katika kuhamasisha pia kwa timu zilizopo Kambini.
  Katika hatua nyingine, TFF imetoa ufafanuzi wa namna ya uuzaji tiketi katika Viwanja vya Mikoani na  Dar es Salaam.
  Katika tiketi zote ambazo zinakatwa katika michezo ya Mikoani zinasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM) na kwa Viwanja vya Dar es Salaam, zoezi hilo linasimamiwa na wamiliki wa Viwanja.
  TFF katika zoezi hilo imekua ikitaja bei ya tiketi na madaraja yake na kuacha kazi kwa mamlaka husika za TAMISEMI na Uwanja kupanga namna ya ukusanyaji wa mapato kupitia tiketi. Hivyo TFF haina dhamana ya kuuza tiketi.
  Aidha, Rais Karia ametuma salamu za rambirambi kwa Familia ya kijana Ibrahim Hassan (7) aliyefariki nje ya uwanja wa Taifa Jumapili Machi 24,2019 katika mchezo wa kutafuta tiketi ya Afcon Tanzania dhidi ya Uganda.
  Rais wa TFF Ndugu Karia,amesema amepokea kwa huzuni taarifa za kijana huyo  ambaye alikuwa na kiu ya kushuhudia mchezo huo.
  Amesema Shirikisho limeumizwa na tukio lililotokea na kusababisha mauti ya kijana huyo. Kwa niaba ya TFF  ametoa pole kwa familia,jamaa,marafiki na wapenzi wa soka. TFF inatoa ubani wa kiasi cha Shilingi 500,000 kwa familia ya kijana huyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS WA TFF WALLACE KARIA AWASHUKURU WATANZANIA KUIUNGA MKONO TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top