• HABARI MPYA

    Tuesday, December 22, 2015

    NIYONZIMA ‘APANGUA’ ADHABU YANGA SC, ATOA VIELELZO TOSHA KUUBANA UONGOZI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amewasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha na kubatilisha adhabu aliyopewa Yanga SC.
    Niyonzima alifungiwa kwa muda usiojulikana Yanga SC wiki iliyopita kwa tuhuma za utovu wa nidhamu baada ya kuchelewa kurejea klabuni, kufuatia ruhusa ya kwenda kuichezea timu yake ya taifa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge nchini Ethiopia mwezi uliopita.
    Hata hivyo, baada ya kuchelewa alirejea akiwa amefungwa plasta gumu (PoP) na kusema aliumia kwenye mashindano hayo, hivyo akabaki Kigali kupata matibabu.
    Haruna Niyonzima (kulia) amewasilisha vielelezo vya kumsafisha Yanga SC dhidi ya adhabu

    Lakini hiyo haikumsaidia kumuepusha na adhabu ya uongozi wa Yanga SC uliokuwa na hasira naye, ukidai imekuwa desturi yake kuchelewa kila anaporuhusiwa kwenda kwao.
    Pamoja na hayo, Niyonzima amewasilisha vielelezo vya barua pepe alizokuwa akituma kwa Katibu Mkuu wa Yanga SC, Dk Jonas Tiboroha ambaye kwa bahati mbaya alikuwa hajibu.
    Amewasilisha pia ushahidi wa vyeti vya Daktari wa timu ya taifa na barua ya Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) vyote vikithibitisha kweli aliumia na alibaki kwa matibabu Kigali.   
    Hii maana yake uongozi wa Yanga SC sasa unaweza kukutana na kulijadili upya suala la mchezaji huyo – maana yake adhabu yake inaweza kutenguliwa.
    Pamoja na hayo, kuna makosa yalifanyika wakati wa kutoa adhabu hiyo, kwani mchezaji hakuitwa kujieleza zaidi ya kuhukumiwa kutokana na historia.  
    Kwa sasa Haruna anaendelea mazoezi peke yake asubuhi na jioni kujiweka fiti, wakati wowote akirejeshwa kikosini awe fiti kuendelea kuisaidia klabu yake katika michuano mbalimbali, hususan Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIYONZIMA ‘APANGUA’ ADHABU YANGA SC, ATOA VIELELZO TOSHA KUUBANA UONGOZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top