• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 18, 2015

  HANS POPPE: WAPINZANI WANAMRUBUNI MAJABVI WAMCHUKUE BAADA YA KUTIBUANA NA MCHEZAJI WAO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba moja ya klabu wapinzani wao, inamrubuni kiungo wao Mzimbabwe Justice Majabvi avunje Mkataba ili wamchukue.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana, Poppe amesema kwamba kiungo huyo amenza visa ambavyo wazi inaonyesha anataka kuvunja Mkataba.
  Na Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba wamekwishajua kilicho nyuma ya jeuri ya mchezaji huyo ni mahasimu wao fulani wanamrubuni.
  “Kuna wapinzani wetu fulani, ambao kwa sasa wapo kwenye mgogoro na mchezaji wao mmoja, sasa wamemrubuni na huyu wa kwetu ili wamchukue badala ya huyo anayewasumbua,”amesema Poppe. 
  Kiungo Justice Majabvi inadaiwa anarubuniwa na wapinzani wa Simba avunje Mkataba

  Mmiliki huyo wa kampuni ya usafirishaji ya Z.H. Poppe amesema kwamba hakuna mgogoro kati yake au klabu na Majabvi, bali mchezaji huyo kwa sasa ‘ameshikwa akili’ na wapinzani.
  “Mimi binafsi huyo mchezaji wala sijawahi hata kuzungumza naye. Aliitwa jana (juzi) na uongozi wala mimi sikuwepo, lakini mambo aliyozungumza ni ya kutufedhehesha na hakuna hata moja kati ya aliyosema yanahusiana na Mkataba wake,” amesema Poppe.
  Ameongeza kwamba Majabvi si Nahodha wa Simba SC na hatakiwi kuzungumza na vyombo vya habari, lakini amefanya hivyo. 
  “Choko choko zote hizi ni …….. (wapinzani), wanakorofishana na ……… (mchezaji wao), sasa wanataka kumchukua huyu ndiyo wanamuambia alete mtafuruku kwetu,” amedai Poppe.
  Hans Poppe amesema kwamba Majbvi analeta chokochoko ili ahamie kwa wa;pinzani wao 

  Kuhusu madai ya nyumba ya kuishi ya Majabvi, Poppe amesema kwamba kiungo alikataa nyumba tatu alizopangiwa na bado uongozi umemuweka kwenye hoteli ya Lamada, Ilala ambako analipiwa Sh 40,000 kwa siku sawa na Sh. Milioni 1.2 kwa mwezi.
  “Cha mno nini. Haya maneno kuwa viongozi hatuwatembelei wachezaji anayasema ya nini na yanahusiana nini na Mkataba wake kama siyo kutafuta kuumbua uongozi,”amesema Poppe na kuongeza;
  “Lakini pia si kweli hatuwatembelei wachezaji, mbona tulikwenda kutoa ahadi wakati wa mapumziko katika mchezo dhidi ya Azam FC (Jumamosi) kwamba tutawapa Sh Milioni 10 wakishinda?” 
  Pamoja na hayo, Poppe amesema kwamba Simba SC ni klabu kubwa na haiwezi kubembeleza mchezaji. “Aende zake, hatubembelezi mtu, tumempa mkataba aupitie na aseme wapi tumekiuka, amekosa na kubaki anasema hataki kuendelea kuchezea Simba sababu hapendi namna klabu inavyoendeshwa. Sasa anataka tuendeshe klabu anavyotaka yeye?” amemalizia kwa kuhoji Poppe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HANS POPPE: WAPINZANI WANAMRUBUNI MAJABVI WAMCHUKUE BAADA YA KUTIBUANA NA MCHEZAJI WAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top