• HABARI MPYA

  Tuesday, December 29, 2015

  SIMBA SC ‘WAPANGUA’ RATIBA KOMBE LA MAPINDUZI, WAWASHITAKI MAREFA TFF

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeomba Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kiusogeze mbele mchezo wake wa ufunguzi Kombe la Mapinduzi dhidi ya Jamhuri ya Pemba uliopangwa kufanyika Januari 2, mwaka huu.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari Dar es Salaam kwamba, hiyo inatokana na klabu yao kuwa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Januari 1, dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.
  “Wazi itatuwia vigumu kucheza mechi Mtwara tarehe moja halafu tarehe mbili tena tucheza mechi nyingine ya Kombe la Mapinduzi. Kwa hiyo tunawaomba ZFA wausogeze mbele mchezo huu,”amesema Manara.
  Simba SC ndiyo mabingwa watetezi Kombe la Mapinduzi

  Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo huo na kikirejea kitaunganisha safari kwenda Zanzibar.
  Aidha, Manara amesema kwamba wamewasilisha malalamiko Bodi ya Ligi juu ya marefa wa mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ambao ulimalizimika kwa sare ya 1-1.
  Amesema katika mchezo huo marefa walipindisha sheria na kuwapendelea wapinzani hao, hivyo wamewasilisha barua ya malalamiko pamoja na ushahidi wa video ya mchezo ili waamuzi hao wachukuliwe hatua.  
  Waamauzi wanaolalamikiwa na Simba SC ni Ngole Mwangole wa Mbeya, Joseph Masija ea Mwanza na Abdallah Rashid wa Pwani.
  Mabingwa hao watetezi, Simba SC wamepangwa Kundi A katika Kombe la Mapinduzi 2016 pamoja na URA ya Uganda, Jamhuri ya Pemba na JKU ya Unguja.
  Mabingwa wa Bara, Yanga SC wamepangwa kundi B pamoja na mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Mtibwa Sugar ya Morogoro na Mafunzo ya Zanzibar.
  Simba SC imepangiwa kufungua dimba na Jamhuri Januari 2, 2016 mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya JKU na URA Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Yanga SC watashuka dimbani siku inayofuata, Januari 3, 2016 kumenyana na Mafunzo, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam FC.
  Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa Januari 9, wakati Fainali itachezwa Januari 13, Uwanja wa Amaan katika kilele cha sherehe za Mapinduzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC ‘WAPANGUA’ RATIBA KOMBE LA MAPINDUZI, WAWASHITAKI MAREFA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top