• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 27, 2015

  HIKI NDICHO KIKOSI CHA AZAM FC KOMBE LA SHIRIKISHO 2016

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imetuma orodha ya wachezaji 27 kwenye Shirikisho la Soka Afrika (CAF), watakaoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
  Azam FC itaanza kampeni ya kuwania taji la michuano hiyo kwa kucheza na mshindi wa jumla wa mchezo kati Bidvest Wits ya Afrika Kusini na moja ya klabu kutoka nchini Seychelles ambayo haijajulikana kwa sasa, zote hizo zikianzia raundi ya awali.
  Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo iliyofanyika Desemba 11 mwaka huu jijini Dakar, Senegal, imeonyesha kuwa Azam FC itaanza kucheza ugenini dhidi ya mojawapo ya timu hizo kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kukipiga nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20.

  Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa na pointi 32, ikizidiwa moja na mabingwa watetezi, Yanga SC, ikifanikiwa kuvuka raundi hiyo itatinga raundi ya pili na kukutana na moja ya timu tatu kati ya Esperance ya Tunisia iliyoanzia raundi ya kwanza, ambayo itatakiwa kupita kwa kucheza na mshindi wa mechi ya raundi ya awali kati ya timu kutoka Chad ambayo haijajulikana na News Stars de Douala ya Cameroon.
  Timu hiyo inayomilikiwa na familia ya Mfanyabiashara maarufu nchini na nje ya mipaka ya Tanzania, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa, itacheza mechi za raundi ya pili kwa kuanzia nyumbani kati ya Aprili 8, 9 na 10 na kuhamia ugenini kati ya Aprili 19 na 20.
  Baada ya mechi za raundi ya pili, CAF itafanya droo ndogo itakayohusisha timu nane zilizobakia kwenye michuano hiyo, ambazo zitapambanishwa na nane nyingine zilizotolewa katika raundi ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupatikana timu nane za mwisho zitakazotinga hatua ya makundi au robo fainali.
  Uongozi wa timu ya Azam FC pamoja na benchi la ufundi, umeweka malengo makubwa kwenye michuano hiyo mwakani ya kufika hatua ya robo fainali, timu hiyo ikiingia hatua hiyo itakuwa ni miongoni mwa timu nane za mwisho zitakazokuwa zikiwania ubingwa huo uliochukuliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka huu.
  Kikosi cha Azam FC CAF; Makipa; Aishi Manula, Ivo Mapunda na Mwadini Ali.
  Mabeki; Pascal Wawa, Aggrey Morris, David Mwantika, Said Mourad, Racine Diouf, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Abdallah Kheri, Gardiel Michael na Waziri Salum.
  Viungo; Himid Mao, Salum Abubakar, Frank Domayo, Jean Mugiraneza, Michael Bolou, Mudathir Yahya, Ramadhan Singano, Farid Maliki, 
  Khamis Mcha na washambuliaji; John Bocco, Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu, Allan Wanga na Ame Ally.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HIKI NDICHO KIKOSI CHA AZAM FC KOMBE LA SHIRIKISHO 2016 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top