• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 18, 2015

  YANGA SC ‘YASHUSHA KIFAA’ HATARI TUPU, MASHABIKI WASEMA NI MKALI KULIKO MNIGER

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji wa Rayon Sport ya Rwanda, Jerome Sina ametua Yanga SC kwa majaribio na leo amevutia mno mazoezini Uwanja wa Boko, kiasi kwamba mashabiki wakasema huyo ni mzuri kuliko Mniger, Issoufou Boubacar Garba.
  Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amemvutia hadi kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na inaelezwa iwapo atafuzu majaribio, atasajiliwa mwishoni mwa msimu.
  Mashabiki wa Yanga SC waliojitokeza kwenye Uwanja wa Boko Veterani leo asubuhi walikiri kwamba Sina, mchezaji wa zamani wa Polisi ya Rwanda na Vilunga FC ya kwao, DRC ni mkali zaidi ya Garba, ambaye leo hakuvutia sana mazoezini tofauti na wakati wa majaribio Tanga.
  Jerome Sina akiwa mazoezini leo Yanga SC Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam

  Tayari Yanga SC imekamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni inayotakiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kama itataka kumsajili Sina, italazimika kumuacha mmoja.
  Beki Mtogo Vincent Bossou anamaliza Mkataba wake wa mwaka mmoja mwishoni mwa msimu, lakini tayari ameingia kwenye kikosi cha kwanza kutokana na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuwa majeruhi.
  Maana yake Bossou anaweza kuongezewa Mkataba iwapo atafanya kazi nzuri katika kipindi hiki cha kumalizia msimu.  
  Wachezaji wengine wote wa kigeni wa Yanga SC bado wana mikataba ya kuanzia mwaka mmoja zaidi, ambao ni beki Mbuyu Twite kutoka DRC, viungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Thabani Kasumoko na washambuliaji Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, Amissi Tambwe wa Burundi na Garba wa Niger.   
  Hata hivyo, Niyonzima kwa sasa anatumikia adhabu ya kusimamishwa na klabu kwa muda usiojulikana kutokana na utovu wa nidhamu.
  Katibu Mkuu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha aliiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kwamba klabu imemsimamisha Niyonzima kwa muda usiojulikana baada ya kurudia kuchelewa kujiunga timu kufuatia ruhusa maalum.
  Dk Tiboroha alisema uamuzi huo umefikiwa na kikao cha Kamati ya Mashindano, chini ya Mwenyekiti wake, Isaac Chanji juzi mjini Dar es Salaam.
  Na amesema hiyo imefuatia Niyonzima kushindwa kujirekebisha licha ya kuonywa mara kadhaa juu ya desturi hiyo isiyopendeza.
  Issoufou Boubacar Garba leo hakuvutia sana mazoezini Uwanja wa Boko
  Jerome Sina akiwa na wachezaji wa Yanga SC mazoezini leo asubuhi  Niyonzima aliibuka mapema wiki hii mjini Dar es Salaam na kujisalimisha klabuni akiwa amefungwa plasta gumu (PoP), maarufu kama ‘hogo’, baada ya Yanga SC kusema itamchukulia hatua za kinidhamu kwa kitendo cha kuchelewa kurejea katika timu.
  Nahodha huyo wa Rwanda aliruhusiwa kwenda kuichezea timu yake ya taifa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge nchini Ethiopia, lakini baada ya mashindano akachelewa kurejea Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC ‘YASHUSHA KIFAA’ HATARI TUPU, MASHABIKI WASEMA NI MKALI KULIKO MNIGER Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top