• HABARI MPYA

    Monday, December 28, 2015

    MILIONEA ALIYEMLETA NIYONZIMA YANGA SC ATOA MAONI YAKE, ASEMA HARUNA…

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MILIONEA Abdallah Ahmed Bin Kleb aliyemleta kiungo Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima Yanga SC, ameunga mkono uamuzi wa kufukuzwa kwa mchezaji huyo.
    Yanga SC leo imevunja Mkataba na kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda kwa madai ya mchezaji huyo wa Amavubi kukiuka vipengele.
    “Mimi kwa kweli ninaunga mkono uamuzi uliochukuliwa na uongozi, kwa sababu suala la nidhamu ni la muhimu mno katika timu. Kama mchezaji ameshindwa kuheshimu Mkataba wake, hii ni hatua sahihi,”amesema Bin Kleb akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jioni ya leo.
    Abdallah Bin Kleb (kushoto) akimkabidhi jezi namba nane Haruna Niyonzima baada ya kukamilisha usajili wake kwa mara ya kwanza mwaka 2011 mjini Kigali, Rwanda

    Aidha, Bin Kleb ambaye alisajili nyota wengine kadhaa Yanga SC akiwemo kiraka Mbuyu Twite, amewataka wapenzi na wanachama wa klabu kuunga mkono uamuzi wa uongozi.
    “Unajua Haruna ni mchezaji mwenye kipaji, ambaye ana wapenzi wengi pale Yanga SC, ambao najua hawataufurahia uamuzi huu. Lakini mimi napenda nichukue fursa hii kuwaomba wana Yanga wote tuungane na uongozi kuafiki hatua hii,”.
    “Mchezaji kama ameshindwa kuheshimu thamani aliyopewa ndani ya klabu, wazi huyo hafai. Haruna tulimchukua kwa Mkataba wa miaka miwili awali, baadaye tukamuongeza miwili. Ikaisha na juzi ametoka kuongezewa mwingine wa miaka miwili,”. 
    “Sasa nadhani amekwishajiona mwenyeji kwenye timu anafanya anavyotaka bila kuzingatia Mkataba wake unasemaje. Ni sahihi tu hatua iliyochukuliwa,”amesema Kleb.
    Aidha, Bin Kleb amesema anaamini hatua iliyochukuliwa itakuwa fundisho kwa wachezaji wengine, ili waweze kuheshimu mikataba yao wakati wote.
    Sakata la kufukuzwa kwa Niyonzima Yanga SC, linaanzia mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia na akachelewa kurejea baada ya mashindano.
    Kufuatia hali hiyo, klabu ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye imekuja na maamuzi magumu.
    Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo amedanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.  
    Haruna ni mchezaji kipenzi cha mashabiki Yanga SC kama anavyoonekana hapa akitunzwa fedha baada ya mechi

    Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
    Na ikamnasa kwenye picha za video siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
    Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MILIONEA ALIYEMLETA NIYONZIMA YANGA SC ATOA MAONI YAKE, ASEMA HARUNA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top