• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 31, 2015

  YANGA SC WAPAA KESHO ZANZIBAR KUFUATA KOMBE LA MAPINDUZI TANGU 2008

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC inafanya mazoezi ya mwisho leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na kesho itapanda boti kwenda Zanzibar kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi.
  Yanga SC imepania kutwaa tena Kombe la Mapinduzi tangu ilipotwaa mara ya mwisho mwaka 2008 na inakwenda Zanzibar na kikosi chake kamili kwa ajili ya vita ya taji hilo.
  Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye mwaka huu timu yake ilitolewa katika Nusu Fainali na JKU hataki kurudia makosa mwakani na amekwishawaambia wachezaji wake hataki mzaha.
  Pamoja na dhamira hiyo, Pluijm amesema ataitumia michuano hiyo kuwainua baadhi ya wachezaji wake aliowapandisha kutoka kikosi cha pili.
  Kikosi cha Yanga SC kinachokwenda kuwania Kombe la Mapinduzi

  “Nitakwenda na kikosi changu kamili, lakini nitabeba na vijana fulani niliowapandisha kutoka timu B ili nikawatafutie nafasi za kucheza kupata uzoefu kidogo,”amesema Pluijm.
  Katika michuano hiyo, Yanga SC imepangwa Kundi B pamoja na Azam FC, Mtibwa Sugar na Mafunzo, wakati Kundi A lina timu za Simba SC, ambao ni mabingwa watetezi, URA ya Uganda, JKU na Jamhuri ya Pemba.
  Yanga SC watafungua dimba la michuano hiyo kwa kucheza na Mafunzo Januari 3, mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam FC usiku.   
  Mabingwa watetezi, Simba SC watateremka uwanjani kwa mara ya kwanza Januari 4, kumenyana na Jamhuri usiku, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya URA na JKU.
  Nusu Fainali zitachezwa Januari 10, wakati Fainali itachezwa Januari 13 sambamba na kilele cha sherehe za Kombe la Mapinduzi 2016. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAPAA KESHO ZANZIBAR KUFUATA KOMBE LA MAPINDUZI TANGU 2008 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top