• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 27, 2015

  MBEYA CITY INAVYOPOTEZA DIRA, SASA IMEKUWA TIMU YA ‘MAFAZA’

  MISIMU miwili iliyopita, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilipokea changamoto mpya nzuri kutoka mkoa wa Mbeya.
  Ilikuwa ni kupanda kwa timu ya Halmashauri ya Mji wa Mbeya, iitwayo Mbeya City Council FC (MCC) ambayo ikishiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza, ilikaribia kuchukua ubingwa.
  Mbeya City wakati huo chini ya kocha Juma Mwambusi, aliyehamia Yanga SC msimu huu, iliongoza Ligi Kuu karibu mzunguko wa kwanza wote, kabla ya kuzidiwa kete na Azam FC na Yanga SC zilimaliza nafasi mbili za juu mwishoni.
  Kuanzia msimu uliofuata, makali ya Mbeya City yakaanza kupotea taratibu na hadi sasa imekuwa timu ya kawaida mno na si tishio tena.

  Katika msimu wake wa kwanza, Mbeya City ilkuwa haifungiki nyumbani Uwanja wa Sokoine na timu zilizofanikiwa japo kupata sare zilikuwa Yanga na Simba.
  Azam FC waliifunga kwa mbinde Mbeya City katika mechi ya mwisho kabisa ya msimu Uwanja wa Sokoine na kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu.
  Lakini mechi ya kwanza Uwanja wa Azam Complex chupuchupu Azam wafungwe kama si kupata sare ya 3-3 katika mchezo mtamu zaidi kuwahi kuchezwa kwenye Uwanja huo.  
  Sasa Mbeya City imekuwa timu ambayo inafungwa popote hata Sokoine. Kwa ujumla Mbeya City imepoteza makali yake kabisa.
  Inawezekana kuna mengi yanachangia kuporomoka kwa Mbeya City, lakini kubwa na linaloonekana ni falsafa yake ya sasa, ambayo ni tofauti na ile waliyokuja nayo miaka mitatu iliyopita.
  Mbeya City ilikuwa timu ambayo inaibua vipaji vyake ndani ya Mbeya na mikoa jirani, ambavyo baadaye vikawa tishio kama akina Deus Kaseke, Paul Nonga ambao sasa wapo Yanga SC na Peter Mwalyanzi wa Simba SC.
  Hakika ilifika wakati watu wakaanza kukumbuka enzi za timu zilizokuwa tishio mjini Mbeya miaka ya nyuma kama Mecco, Tukuyu Stars na Tiger kutokana na makali ya Mbeya City, ikiundwa na asilimia kubwa ya wachezaji wa nyumbani kama akina Mwagane Yeya.
  Lakini sasa Mbeya City si ile tena ya kuibua vipaji vya nyumbani, bali imekuwa ni timu ya kusajili wachezaji wakongwe ambao wameshindikana katika timu kubwa za mjini.
  Kuwa na wakongwe wachache katika timu si vibaya, lakini hali ilvyo sasa ndani ya Mbeya City si kawaida, imekuwa timu ya ‘mafaza’.
  Makipa wote, Hannington Kalyesebula na Juma Kaseja ni ambao wametumika kwa muda mrefu katika klabu zao za awali.
  Haruna Shamte, Juma Nyosso, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Haruna Moshi ‘Boban’ na Themi Felix hawa ni baadhi tu ya wachezaji waliosajiliwa Mbeya City siku za karibuni.
  Wakati huo huo, mshambuliaji Mwagane Yeya ameachwa katika timu kwa sababu ambazo hazieleweki, huku timu ikipoteza nyota wengine kama Kaseke, Mwalyanzi, Nonga na Saad Kipanga.
  Hapo ndipo unapoona kabisa Mbeya City imepoteza dira yake nzuri iliyoingia nayo katika Ligi Kuu ya nchi hii miaka mitatu iliyopita.
  Vyema sasa uongozi ukashituka na wakati wakipigania kubaki Ligi Kuu msimu huu, wanapaswa kujipanga upya kuelekea msimu ujao.
  Mbeya pekee ni mkoa wenye vipaji vingi ambavyo Mbeya City wanaweza kuvitumia kujirudisha juu.
  Yanga SC ya Dar es Salaam iliweza kumsajili winga Godfrey Mwashiuya kutoka timu ya Kemondo, lakini Mbeya City ikasafiri kuifuata saini ya Haruna Moshi ‘Boban’ mjini.
  Nirudie, si vibaya kuwa na wakongwe japo wawili kikosini, ili wawaongoze vijana, lakini hali ilivyo sasa katika kikosi cha Mbeya City inajionyesha tu si sawa.
  Na huwezi kustaajabu Mbeya City imevuna pointi 11 katika mechi 13 ikiwa kikosini imesheheni ‘mafaza’ walioshindikana timu za mjini. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBEYA CITY INAVYOPOTEZA DIRA, SASA IMEKUWA TIMU YA ‘MAFAZA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top