• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 31, 2015

  SIMBA SC WALALAMIKA KUFANYIWA FUJO, KUPIGWA MAWE MAZOEZINI MTWARA LEO

  Na Mwandishi Wetu, MTWARA
  WACHEZAJI wa Simba SC wamefanyiwa vurugu leo asubuhi wakati wakifanya mazoezi Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya wenyeji, Ndanda FC.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba vurugu hizo zimefanywa na mashabiki wanaosadikiwa kuwa wa Ndanda.
  “Tulikuwa kwenye mazoezi asubuhi katika maandalizi yetu ya mchezo wa kesho. Ghafla likatokea kundi la mashabiki na kuanza kutufanyia fujo ikiwemo kuwapiga mawe wachezaji,”amesema Manara.
  Hali ilivyokuwa leo asubuhi baada ya wachezaji wa Simba SC kufanyiwa vurugu

  Mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Yanga SC, Sunday Manara ‘Kompyuta’ amesema bahati nzuri hakuna mchezaji aliyeumia na baadaye walifanikiwa kuwakamata watu kadhaa waliohusika na vurugu hizo na kuwapeleka Polisi.
  Manara ambaye kaka wa baba yake, Kitwana Manara pia alicheza Yanga, amelaani vurugu hizo na kusema zinachafua sura ya mkoa wa Mtwara na klabu ya Ndanda.
  “Ndanda inashiriki Ligi Kuu, na mechi zote haichezi hapa Nangwanda Sijaona pekee, wanasafiri na kwenda mikoani pia. Wapi walifanyiwa fujo?,”amehoji Manara.
  Aidha, Manara amesema Chama cha Soka Mtwara kinapaswa kuwaelimisha mashabiki wake wakaachana na mambo hayo ya kizamani.
  “Imenikitisha sana. Mimi Mtwara ni moja ya mikoa ambayo ninaiheshimu sana,” amesema. “Imetoa wachezaji wakubwa sana wa nchi hii kuanzia enzi za akina Mohammed Chuma, Juma Mkambi (wote marehemu), Mohammed Hussein, Idelphonce Amlima na wengine,”ameongeza.
  Pamoja na yote, Manara amesema Simba SC iko vizuri kuelekea mchezo wa kesho na vurugu walizofanyiwa zimewatia hamasa zaidi wachezaji ili kesho walipe kisasi kwa kuifunga Ndanda.
  Mchezo wa Simba na Ndanda utahitimisha awamu fulani ya Ligi Kuu kabla ya kwenda mapumzikoni tena hadi katikati ya Januari, kupisha Kombe la Mapinduzi, michuano inayoanza Janauri 3 visiwani Zanzibar. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WALALAMIKA KUFANYIWA FUJO, KUPIGWA MAWE MAZOEZINI MTWARA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top