• HABARI MPYA

  Saturday, December 19, 2015

  AZAM FC KURUDI KILELENI LIGI KUU LEO? YANGA INA KAZI NA STAND UNITED YA MAGURI ‘MABAO’, SIMBA SC NA KIBOKO YAO TOTO AFRICANS…

  RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
  Leo; Desemba 19, 2015
  Yanga SC vs Stand United
  Mwadui FC vs Ndanda FC
  Kagera Sugar vs African Sports
  Prisons vs Mtibwa Sugar
  Toto Africans vs Simba SC
  Majimaji vs Azam FC
  Desemba 20, 2015
  JKT Ruvu vs Coastal Union
  Mbeya City vs Mgambo JKT
  Kikosi cha Azam FC leo kinamenyana na Majimaji mjini Songea

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  AZAM FC inamenyana na Majimaji Uwanja wa Majimaji mjini Songea leo katika mchezo ambao ikishinda inarejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Azam FC ilishushwa kileleni na mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumatano.
  Lakini leo Azam FC inakutana na Majimaji ambayo mchezo wa mwisho ilifungwa 5-1 na vibonde wenzao Toto Africans Uwanja wa Majimaji.
  Azam FC inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, kutokana na ukweli kwamba Majimaji ni timu dhaifu.
  Mabingwa watetezi, Yanga SC nao pia watashuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo kumenyana na Stand United ya Shinyanga, ambayo hakika na timu ngumu.
  Ikitoka kufungwa 2-0 nyumbani na Mwadui katika mchezo wake uliopita, Stand inayoongozwa na kinara wa mabao wa Ligi Kuu, Elias Maguri inatarajiwa kupambana leo kuzinduka.
  Nao mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC watakuwa Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza leo kumenyana na Toto Africans. 
  Toto imekuwa na kawaida ya kuifunga Simba SC Uwanja wa Kirumba na hilo linafanya mchezo wa leo, uvute hisia za wengi. 
  Simba SC leo wanatarajiwa kuwa kamili, baada ya wachezaji wake iliyowaingiza dirisha dogo, Mganda Brian Majwega, Mkenya Paul Kiongera na wazalendo Novat Makunga na Hajji Ugando kuruhusiwa kucheza.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni kati ya Mwadui FC na Ndanda FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Kagera Sugar na African Sports Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na Prisons na Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya – wakati kesho JKT Ruvu wataikaribisha Coastal Union Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam na Mbeya City watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Sokoine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC KURUDI KILELENI LIGI KUU LEO? YANGA INA KAZI NA STAND UNITED YA MAGURI ‘MABAO’, SIMBA SC NA KIBOKO YAO TOTO AFRICANS… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top