• HABARI MPYA

    Thursday, December 24, 2015

    AZAM FC YAPANIA KUMALIZA MWAKA IKIWA KILELENI LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imejiwekea malengo ya kushinda mechi mbili zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ili kurejea kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.
    Azam FC inashika nafasi ya pili kwa sasa ikiwa na pointi 29 ikizidiwa pointi moja na Yanga iliyo kileleni kwa pointi 30, waliocheza mchezo mmoja zaidi ya Azam, ambayo itarejea kileleni kama ikizifunga Kagera Sugar Jumapili hii na Mtibwa Sugar Jumatano ya wiki ijayo.
    Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema jana kwamba katika kuhakikisha hilo linatimia timu hiyo itaingia kambini kesho alasiri hadi watakapomaliza kucheza na Mtibwa Sugar wiki ijayo.

    “Tumedhamiria kurejea kwenye nafasi yetu kileleni, hilo litatimia kama tukishinda mechi zetu mbili zijazo (Kagera Sugar, Mtibwa Sugar), katika kuhakikisha hilo linatimia kama tulivyopanga, timu itaingia kambini kesho na itamalizika mara baada ya mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar,” alisema.
    Hall alisema kuwa anataka kuiona Azam FC ikimaliza mwaka huu ikiwa kileleni mwa ligi, yote hayo ni kutimiza malengo ya timu hiyo ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu, walioutwaa kwa mara ya kwanza na mwisho msimu wa 2013/14 bila kufungwa mchezo wowote.
    Mwingereza huyo aliongeza kuwa mara baada ya kambi hiyo, atawapa mapumziko ya sherehe za mwaka mpya wachezaji wake na watatakiwa kuripoti kambini Januari Mosi mwakani na siku hiyo hiyo mchana itaanza safari ya kuelekea visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.
    Katika mazoezi ya jana asubuhi, benchi la ufundi la Azam FC lilikuwa likiwapa mazoezi ya kuwaweka fiti wachezaji, wakianza kukimbia taratibu na baadaye kasi kwa kuzunguka uwanja, pamoja na mbinu watakazotumia katika mechi hizo.
    Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, itaingia kwenye mechi hizo ikiwa na hali nzuri kabisa, kwani mpaka sasa imepata ushindi wa asilimia 100 kwenye uwanja wa nyumbani, huku Jumapili iliyopita ikitoka kuichapa Majimaji ya Songea mabao 2-1 ugenini mkoani Ruvuma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAPANIA KUMALIZA MWAKA IKIWA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top