• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 28, 2015

  ENYIMBA WAMTUPIA VIRAGO KOCHA ALIYEWAPA UBINGWA WA NIGERIA

  Kadiri Ikhana amefukuzwa Enyimba
  MABINGWA wa Nigeria, Enyimba wanatarajiwa kutaja kocha mpya baada ya kumfukuza aliyekuwa kocha wao Mkuu, Kadiri Ikhana.
  Ikhana hakuongezewa Mkataba baada ya kuwapa Tembo wa Watu taji la saba la Ligi Kuu ya Nigeria mwishoni mwa msimu wa 2014/15.
  Ofisa wa klabu hiyo, Farriel Alaputa amesema kwamba uongozi utatangaza kocha mpya wa mabingwa hao mara mbili wa Afrika kuelekea msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa na mashindano ya nyumbani.
  “Mtu mpya atateuliwa siku zijazo kuchukua nafasi ya kocha Mkuu wa zamani, Kadiri Ikhana ambaye hakuongezewa Mkataba kwa sababu ambazo uongozi unajua. Uongozi umeamua kuipatia timu kocha atakayefaa kwa ajili ya kushinda mataji zaidi ya bara na nchini,” amesema Alaputa.
  Hata hivyo, Alaputa hakuthibitisha tetesi kwamba mabingwa hao mara saba Nigeria watamrejeha kocha wao wa zamani, Salisu Yusuf.
  “Siwezi kuthibitisha hilo kwa sasa kwamba Salisu Yusuf ameteuliwa kuchukua nafasi ya Kadiri Ikhana, nina uhakika haitachukua muda mrefu kumtambulisha kocha mpya wa Enyimba,” amesema Alaputa.
  Enyimba tayari imepangwa kuanza na mabingwa wa Uganda, Vipers katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wiki ya pili ya Februari mjini Kampala.
  Kocha huyo wa zamani wa Kano Pillars na Kwara United, aliiwezesha Enyimba kushinda taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ENYIMBA WAMTUPIA VIRAGO KOCHA ALIYEWAPA UBINGWA WA NIGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top