• HABARI MPYA

    Sunday, December 20, 2015

    SIMBA SC IMEKUWA YA ‘KUCHEZEWA CHEZEWA’ NA MTU YEYOTE!

    KIUNGO Mzimbabwe, Justice Majabvi hakusafiri na timu kwenda Mwanza kucheza mchezo dhidi ya Toto Africans jana.
    Na sababu ana mgogoro na klabu yake, ambao bila kusita nauita usio na kichwa wala miguu na viongozi wamekubali kuwa dhaifu kwa mchezaji.
    Baada ya kuichezea Simba SC mechi 20 za mashindano yote na kuifungia bao moja, Majabvi ameibua mgogoro wa kijinga kabisa.

    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe, kiungo huyo aliyetua Msimbazi Julai mwaka huu, aliwatolea maneno ya kufedhehesha viongozi baada ya kuitwa kwenye kikao cha kujadili malalamiko yake aliyotoa kwenye vyombo vya habari.
    Poppe amesema Majabvi alizungumza maneno ya kufedhehesha uongozi na hakuna hata moja kati ya aliyosema yanahusiana na Mkataba wake.
    Kuhusu madai ya nyumba ya kuishi ya Majabvi, Poppe amesema kwamba kiungo alikataa nyumba tatu alizopangiwa na bado uongozi umemuweka kwenye hoteli ya Lamada, Ilala ambako analipiwa Sh 40,000 kwa siku sawa na Sh. Milioni 1.2 kwa mwezi.
    “Cha mno nini. Haya maneno kuwa viongozi hatuwatembelei wachezaji anayasema ya nini na yanahusiana nini na Mkataba wake kama siyo kutafuta kuumbua uongozi,”alisema Poppe.
    “Lakini pia si kweli hatuwatembelei wachezaji, mbona tulikwenda kutoa ahadi wakati wa mapumziko katika mchezo dhidi ya Azam FC (Jumamosi) kwamba tutawapa Sh Milioni 10 wakishinda?” 
    Pamoja na hayo, Poppe amesema kwamba Simba SC ni klabu kubwa na haiwezi kubembeleza mchezaji. “Aende zake, hatubembelezi mtu, tumempa mkataba aupitie na aseme wapi tumekiuka, amekosa na kubaki anasema hataki kuendelea kuchezea Simba sababu hapendi namna klabu inavyoendeshwa. Sasa anataka tuendeshe klabu anavyotaka yeye?” alimalizia kwa kuhoji Poppe.
    Basi huu ndiyo mgogoro wa Simba SC na Majabvi na hatimaye jana mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza tangu mwanzo wa msimu alikosekana timu ikitoa sare ya 1-1.
    Kinachonipa wasiwasi na maelezo ya Poppe, kumuambia mchezaji mwenye Mkataba na timu aende zake tu wakati amesajiliwa kwa fedha.
    Inawezekanaje, mchezaji asajiliwe na klabu kwa kusaini yeye mwenyewe Mkataba na baada ya miezi mine, asema haridhishwi na jinsi klabu inavyoendeshwa, anataka kuondoka.
    Hii inawezekana kwa Simba SC na tena Poppe anasema kabisa kwamba mchezaji huyo anarubuniwa klabu moja wapinzani wao avunje Mkataba ili wamchukue.
    “Kuna wapinzani wetu fulani, ambao kwa sasa wapo kwenye mgogoro na mchezaji wao mmoja, sasa wamemrubuni na huyu wa kwetu ili wamchukue badala ya huyo anayewasumbua,”alisema Poppe. 
    Kama hivyo ndivyo, Simba SC ikiwa ina haki zote za kummiliki mchezaji huyo imechukua hatua gani?
    Majabvi anapaswa kuwa kazini Simba SC hata kama ana madai yoyote aendelee nayo, lakini autumikie Mkataba wake aliosaini Julai.
    Nashindwa kuwaelewa viongozi wa Simba SC chini ya Rais wake, Evans Aveva – wameifanya klabu imekuwa ya kuchezewa na mtu yeyote. Huu ni udhaifu, tena mkubwa sana. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC IMEKUWA YA ‘KUCHEZEWA CHEZEWA’ NA MTU YEYOTE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top