• HABARI MPYA

  Thursday, December 17, 2015

  KIONGERA RUKSA KUCHEZA SIMBA SC, ATAANZA NA ‘TOTO LA YANGA’ JUMAMOSI CCM KIRUMBA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Paul Kiongera (pichani kulia) sasa ataanza kuichezea klabu yake katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Mkenya huyo alishindwa kuichezea Simba SC ikitoa sare ya 2-2 na Azam FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka asubiri muda wa pingamizi upite.
  Lakini baada ya TFF kufanyia marekebisho ya kanuni za usajili na sasa mchezaji ambaye amesajiliwa katika mfumo wa mtandao wa (Transfer Matching System), maarufu kama TMS anapewa leseni moja kwa moja kuanza kuchezea timu mpya, Kiongera atacheza.
  TFF imesema itatoa leseni ya usajili wa mchezaji ambaye amethibitishwa kupitia mtandao wa TMS baada ya kuwepo nyaraka zote; mkataba uliomalizika, barua ya kuvunja mkataba, barua ya kuachwa (release letter), mkataba mpya na uthibitisho wa makubaliano kati ya klabu zinazohusika.
  “Licha ya mchezaji kupata leseni, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji bado itakuwa na mamlaka ya kushughulia upungufu, malalamiko ya kiusajili, pingamizi na uhalali wa kimkataba kati ya pande mbili (mchezaji na klabu),”imesema taarifa ya TFF na kuongeza; 
  “Wachezaji wote wa kigeni waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) wanapaswa kulipiwa dola za kimarekani 2,000 kwa kila mmoja kabla ya kupatiwa leseni na kuanza kuzitumikia klabu zao katika michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho,”.
  Aidha, TFF pia kupitia kamati ya sheria na hadhi za wachezaji inaweza kumruhusu kwa kipindi maalum mchezaji mwenye dosari acheze kwa leseni ya muda (provisional license) hadi dosari hizo kati ya klabu na klabu zitakapomalizwa. Iwapo dosari hizo hazitakuwa zimemalizwa, mchezaji anaweza kuzuiwa kucheza na klabu husika kuadhibiwa.
  TFF imezitaka timu zote za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kufuatilia ili kujua wachezaji ambao hawana pingamizi na leseni za wachezaji waliopitishwa wanaweza kuanza kutumika kuanzia kesho tarehe 18/12/2015 na kwenye michezo ya kombe la Shirikisho (FA Cup) kama hawakuwa wamecheza raundi ya kwanza kwenye klabu ya zamani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIONGERA RUKSA KUCHEZA SIMBA SC, ATAANZA NA ‘TOTO LA YANGA’ JUMAMOSI CCM KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top