• HABARI MPYA

  Wednesday, December 23, 2015

  MAJABVI AJISALIMISHA SIMBA SC, AGHAIRI UASI, AREJEA KUNDINI MSIMBAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO Mzimbabwe, Justice Majabvi (pichani kulia) ameomba kurejea kwenye klabu yake, Simba SC baada ya kutafakari upya uamuzi wake wa awali wa kutofanya mazoezi na wenzake.
  Majabvi alisusa kuendelea kuichezea Simba SC akidai haridhishwi namna ambavyo klabu inaendeshwa, lakini leo amejiunga na wenzake kambini mjini Mwanza.
  Simba ipo Mwanza ikijiandaa ya mchezo wake ujao wa  Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Jumamosi.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Hajji Manara amesema kwamba pamoja na klabu kumpokea na kumruhusu mchezaji huyo kwenda Mwanza, imelifikisha suala lake katika Kamati ya Nidhamu ya klabu.
  Manara amesema kwamba wanatarajia hatua za stahili zitachukuliwa kwa Majabvi.
  Mapema wiki hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe aliiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba Majabvi amekatwa mshahara kwa kitendo cha kuzungumza na vyombo vya Habari, jambo ambalo ni kinyume cha Mkataba wake.
  Aidha, Poppr alisema pia mchezaji huyo anatarajiwa kupewa adhabu nyingine, kwa kitendo cha kutoonekana kwenye mazoezi kwa zaidi ya wiki mbili.
  Simba SC inaamini mchezaji wake huyo anarubuniwa na moja ya klabu wapinzani wao avunje Mkataba ili wamchukue – na Poppe amesema Majabvi amenza visa ambavyo wazi inaonyesha anataka kuvunja Mkataba.
  “Kuna wapinzani wetu fulani, ambao kwa sasa wapo kwenye mgogoro na mchezaji wao mmoja, sasa wamemrubuni na huyu wa kwetu ili wamchukue badala ya huyo anayewasumbua,”amesema Poppe. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAJABVI AJISALIMISHA SIMBA SC, AGHAIRI UASI, AREJEA KUNDINI MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top