• HABARI MPYA

    Wednesday, December 16, 2015

    MKUTANO MKUU TFF WAAHIRISHWA, SHIRIKISHO HALINA FEDHA ‘LIMEFULIA MBAYA’

    Rais wa TFF, Jamal Malinzi yuko katika wakati mgumu kwa sasa
    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MKUTANO Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliokuwa ufanyike mwishoni mwa wiki mjini Tanga, sasa hautakuwepo.
    BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TFF wametumiwa ujumbe mchana huu kutaarifiwa kwamba Mkutano huo hautakuwepo.
    Na sababu ni ukosefu wa fedha, baada ya kufungwa kwa akaunti zote za TFF kutokana na madeni ya kodi wanayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
    Hili linakuwa pigo la pili kwa TFF, baada ya awali kusitisha ziara ya timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15) Afrika Mashariki.
    Mwishoni mwa mwezi Novemba 2015, TRA Ilala ulitoa agizo la kufungwa na kuchukuliwa fedha kutoka kwenye akaunti za TFF ili kulipa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.6, sehemu kubwa ikiwa ni malipo ya kutoka kwenye mishahara (PAYE) ya makoch Jan Poulsen, Kim Poulsen, na Jacob Michelsen na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo kati ya Tanzania na Brazil mwaka 2010.
    Baada ya hatua hiyo TFF iliwasiliana na TRA na kuweka bayana kwamba deni la walimu (makocha) na mchezo dhidi ya Brazil lilistahili kulipwa na serikali na haikuwa sahihi kulielekeza TFF.
    Aidha TFF ilieleza athari ambazo zingetokea iwapo amri hiyo (Agent Order) ingetekeleezwa kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa ziara ya timu ya vijana chini ya miaka 15 (U15) katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, kusimama kwa program za vijana na wanawake, Mkutano Mkuu, Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Shirikisho.
    Baada ya utekelezaji wa amri hiyo kuanza TFF ilifanya kikao na TRA na makubaliano ya kufungua akaunti yakafanikiwa. Hata hivyo akaunti zilifunguliwa zikiwa hazina fedha kwa kuwa zilishapelekewa Benki Kuu (BOT) na zoezi la madai haliwezi kukamilika kwa muda mfupi.
    Baada ya hali hiyo kujitokeza, TFF ilifanya kila linalowezekana kuhakikisha Mkutano Mkuu unafanyika ikiwa ni pamoja na kutafuta ufadhili toka kwa  wadau wake, lakini zoezi hilo limeshindikana katika muda mfupi uliopo na hivyo Shirikisho  limeamua kuahirisha Mkutano Mkuu 2015 mpaka hapo hali itakaporuhusu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKUTANO MKUU TFF WAAHIRISHWA, SHIRIKISHO HALINA FEDHA ‘LIMEFULIA MBAYA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top