• HABARI MPYA

    Tuesday, December 29, 2015

    MAGURI NDIYE MKALI WA MABAO TANZANIA KWA SASA, AWAPELEKA PUTA WAGENI LIGI KUU

    WANAFUKUZANA KWA MABAO LIGI KUU
    1: Tambwe Amissi 10
    2: Elias Maguri 9
    3: Donald Ngoma 8
    4: Hamisi Kiiza 8
    5: Kipre Tchetche 8
    6: Paul John Nonga 5
    7: John Bocco 5
    8: Ibrahim Hajib 5
    Elias Maguri (kushoto) akiwa na Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' baada ya kufunga bao katika mchezo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Algeria katika sare ya 2-2 Dar es Salaam mwezi uliopita 

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZAJI wa Stand United ya Shinyanga, Elias Maguri ameendelea kuwawakilisha vizuri washambuliaji wazalendo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Mfungaji huyo wa bao la kwanza katika sare ya 2-2 na Algeria mchezo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Dunia, anapambana na washambuliaji wa kigeni watupu katika nafasi tano za juu kwenye mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu, akiwa anashika nafasi ya pili sasa baada ya kuongoza kwa muda mrefu.
    Maguri sasa anazidiwa kwa bao moja tu na mshambuliaji wa Yanga SC, Mrundi Amissi Tambwe mwenye mabao 10. 
    Maguri aliyejiunga na Stand United msimu huu baada ya kuchwa na Simba SC, anamzidi kwa bao moja Mzimbabwe Donald Ngoma wa Yanga SC mwenye mabao nane sawa na Mganda wa Wekundu wa Msimbazi, Hamisi Kizza ‘Diego’ na Muivory Coast wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche.
    Ikumbukwe kocha wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr aliagiza Maguri aachwe Simba SC kwa madai anakosa sana mabao na Stand United ‘ikajiokotea dhahabu mchangani’ na sasa inajivunia matunda ya mshambuliaji huyo.
    Wachezaji wengine wa Tanzania wanaojitutumia katika mbio za ufungaji bora ni mshambuliaji Fully Zully Maganga wa JKT Mgambo, beki Shomari Kapombe wa Azam FC wenye mabao manne sawa na kiungo Mzimbabwe, Thabani Michael Kamusoko, wakati washambuliaji Atupele Green Jackson, Simon Happygod Msuva mfungaji bora wa msimu uliopita na Jerry Tegete wa Mwadui FC kila mmoja ana mabao matatu sawa na Mrundi wa Azam FC, Didier Kavumbagu.
    Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara bado mbichi, Raundi 13 tu zikiwa zimechezwa maana yake hata mzunguko wa kwanza haujakamilika – maana yake mbio za ufungaji bora bado ndefu. Nani atarithi kiatu cha Msuva msimu huu? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAGURI NDIYE MKALI WA MABAO TANZANIA KWA SASA, AWAPELEKA PUTA WAGENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top