• HABARI MPYA

  Sunday, December 20, 2015

  TAMBWE: NACHEZA, NAFUNGA LAKINI SINA AMANI MOYONI

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, Amissi Joselyn Tambwe amesema kwamba anacheza na kufunga mabao Yanga SC, lakini hana amani moyoni.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana, Tambwe amesema kwamba na kinachomnyima amani ni mauwaji ya Kimbari yanayoendelea nchini Burundi.
  “Kwa kweli kama hali itaendelea hivi, nitalazimika kuileta familia yangu hapa (Dar es Salaam), sina raha kabisa. Mimi niko huku, lakini kule kila siku watu wanakufa,”amesema.
  Na Tambwe akasema mabao matatu aliyofunga jana Yanga ikiilaza Stand United 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni zawadi mwanawe.
  Amissi Tambwe akiondoka na mpira wake jana baada ya kukabidhiwa kufuatia kufunga hat trick

  “Nilizungumza na mwanangu jana (juzi) na akanitakia kila heri katika mchezo wa leo. Nami mabao haya ni zawadi yake,”amesema.
  Amani imechafuka nchini Burundi, kutokana na mapigano baina ya Jeshi la Serikali na kundi la waasi. 
  Tayari Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limepitisha azimio la kuwatuma wanajeshi wake 5000 nchini Burundi ili kuzuia mlipuko wa mauaji hayo ya Kimbari nchini humo, ambayo yanahofiwa kutokea wakati wowote.
  Uamuzi huo umechukuliwa ikiwa ni wiki moja tu tangu kutokea kwa mauaji ya watu zaidi 90 mjini Bujumbura na kuacha mamia wengine wakiwa wamejeruhiwa
  Vikosi vya usalama na ulinzi pamoja na wanamgambo wa chama tawala cha CNDD-FDD wananyooshewa kidole kutekeleza kwa makusudi mauaji hayo.
  Mauaji hayo yalitokea baada ya zaidi ya saa nne ya mapigano katika kambi tatu za jeshi mjini Bujumbura baada ya wananchi wanaopinga utawala wa Rais Pierre Nkurunziza kuvamia makambi ya jeshi.
  Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetoa siku nne kuanzia juzi kwa serikali ya Burudi kutafakari azimio hilo, na iweze kutoa jibu sahihi, la sivyo Baraza hilo linasema litatumia nguvu kulingana na uwezo linalopewa na Katiba yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAMBWE: NACHEZA, NAFUNGA LAKINI SINA AMANI MOYONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top