• HABARI MPYA

  Tuesday, July 10, 2018

  TEGETE, LUHENDE NA WAKALI WENGINE WATANO WA NDANDA FC WASAINI KAGERA SUGAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Kagera Sugar ya Bukoba imefanya usajili wa kishindo wa wachezaji wapya saba kutoka timu mbalimbali kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Wachezaji hao wapya ambao kila mmoja amesaini mkataba wa mwaka mmoja ni pamoja na watano kutoka Ndanda FC ya Mtwara ambao ni kipa Jeremiah Kasubi, mabeki Hemed Khoja, Ahmad Waziri, kiungo Majid Khamis na mshambuliaji Omary Mponda.
  Wengine ni wachezaji wa zamani wa Yanga SC, beki David Luhende kutoka Mwadui FC na mshambuliaji Jerson Tegete kutoka Maji Maji ya Songea.
  David Luhende (kulia) amesaini mkataba wa mwaka mmoja Kagera Sugar 


  Mshambuliaji Jerry Tegete amejiunga na Kagera Sugar ya Bukoba akitokea Maji Maji ya Songea

  Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amechukua hatua ya mapema kusajili wachezaji wapya wa kutosha kufuatia kuondokewa na nyota wake kadhaa.
  Wachezaji walioondoka ni pamoja na kipa Juma Kaseja aliyehamia KMC, beki Mohammed Faki, kiungo Ally Nassor ‘Ufudu waliohamia JKT Ruvu za Dar es Salaam na mshambuliaji Jaffar Kibaya aliyehamia Mtibwa Sugar ya Morogoro. 
  Kagera Sugar ilimaliza Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika nafasi ya tisa baada ya kujikusanyia pointi 37 katika mechi 30 za msimu uliopita.
  Lakini Kagera Sugar zaidi inajivunia kuwa timu pekee iliyowafunga mabingwa, Simba SC 1-0 Mei 19 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam mbele ya Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, John Pombe Joseph Magufuli. Ni siku hiyo ambayo, Rais Magufuli aliwakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Simba SC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TEGETE, LUHENDE NA WAKALI WENGINE WATANO WA NDANDA FC WASAINI KAGERA SUGAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top