• HABARI MPYA

  Monday, July 02, 2018

  KAGERE AING’ARISHA SIMBA TAIFA, SINGIDA UNITED NAYO YAZIDI KUTAKATA KATIKA KOMBE LA KAGAME

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  SIMBA na Singida United ya mkoani Singida zimeendeleza wimbi la ushindi katika michuano ya Kombe la Kagame.
  Singida United ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata ushindi baada ya mchana wa leo kuifunga Dakadaha FC ya Somalia bao 1-0 katika mchezo wa Kundi C la michuano hiyo kwenye Uwanja wa Azam Complex.
  Mchezo huo ulifuatiwa na mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Simba na APR saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mabingwa hao wa Tanzania Bara wakashinda mabao 2-1.
  Katika mchezo huo, bao pekee la Singida United ambayo awali iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1, lilifungwa na Habibu Kiombo katika dakika ya 54 akimalizia pasi ya Eliuter Mpepo.

  Dakadaha ambayo awali ilifungwa na Simba mabao 4-0, angalau leo imeonyesha uhai kwa kuweza kuizuia Singida United isipate ushindi mkubwa kama ilivyotarajiwa na wengi.
  Nayo Simba ikiwatumia wachezaji wake wapya akiwemo Meddie Kagere, Pascal Wawa na Adam Salamba, imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya APR katika mchezo mwingine wa Kundi C.
  APR ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 66 mfungaji akiwa Nkinzingabo Fiston aliyepokea pasi Byiringiro Lague, Simba ilisawazisha bao hilo dakika ya 72 mfungaji akiwa ni Adam Salamba aliyemalizia pasi ya Marcel Kaheza.
  Simba ilipata bao lake la pili dakika ya 90 kwa njia ya penalti mfungaji akiwa ni Meddie Kagere.
  Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kubaki kileleni mwa Kundi C, ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na Singida United pia ikiwa na pointi sita lakini imezidiwa tofauti ya mabao na Simba.
  APR ipo nafasi ya tatu ikiwa haina pointi kama Daladaha inayoshika mkia ambayo awali ilidai inaihofia Simba tu katika kundi lao.
  Katika michezo ya jana jioni ya Kundi A iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, JKU ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Kator FC ya Sudani Kusini huku  Vipers ya Uganda ikitoka sare ya bao 1-1 na mabingwa watetezi Azam FC. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERE AING’ARISHA SIMBA TAIFA, SINGIDA UNITED NAYO YAZIDI KUTAKATA KATIKA KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top