• HABARI MPYA

  Monday, April 01, 2024

  SERIKALI YASAFIRISHA MASHABIKI 48 KWENDA KUISHANGILIA AFRIKA KUSINI


  SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejitolea kusafirisha mashabiki 48 wa klabu ya Yanga kwa basi kwenda Jijini Pretoria, Afrika Kusini kuishangilia timu hiyo katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Yanga SC watakuwa wageni wa Mamelodi Sundowns Ijumaa kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria wakihitaji ushindi au sare ya mabao ili kwenda Nusu Fainali kufuatia sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA' amesema kwamba mashabiki hao wameanza safari yao mapema leo na kwamba safari hiyo imegharimiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo na kutoa ushirikiano kwa uwekezaji binafsi kwenye sekta ya michezo.
  "Kwanza niwapongeze sana kwa uamuzi wa kusafiri kwa basi kwani mngeweza kusema mbaki nyumbani na kutazama mechi kwenye Tv, Hii inamaanisha nyinyi ni wafia Yanga, Hongereni sana. Uzuri kiwango cha timu yetu mmekiona na kinaridhisha, mpinzani tunayekwenda kucheza naye hana faida ya Mashabiki wengi hivyo naamini Nguvu ya kushangilia ambayo mnayo itakwenda kuleta tija kwenye mchezo wetu siku ya ijumaa," amesema Mwinjuma.
  "Nimekuja hapa kufikisha salamu za Serikali chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan, kila kinachoendelea yeye anafuatilia kwa umakini na anawatakia kila la heri kwenye Safari hii na kwenye mchezo wetu siku ya ijumaa,".
  "Nilitamani niliseme hili na nachukua nafasi hii kulisema, sisi Mashabiki huwa tunashangilia matukio tu, nafikiri hali hii kama Wachezaji wana masikio ya kuwasilikiza Mashabiki basi inaweza kuwavunja moyo, hivyo niwashauri tuendelee kujifunza Utamaduni wa kushangilia muda wote na niwaombe tukienda Uwanjani tuwe tunashangilia kuanzia mwanzo wa mchezo mpaka mwisho kwani itatusaidia kuwa na mchezo mzuri,".
  "Tunakuwa pamoja nanyi wakati wote kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa na nina uhakika tutaiwakilisha nchi yetu vizuri kwasababu tuna timu bora, niwatakie Safari Njema," amesema Naibu Waziri, Mwinjuma
  Kwa upande wake Rais wa Yanga SC, mashabiki hao wamepata nafasi hiyo baada ya uongozi wa klabu kuiomba Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wake, Dk. Damas Ndumbaro na ameishukuru Wizara kwa kukubali Ombi hilo.
  "Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na shilingi laki 6 na tulipata watu 30, niwahakikishie baada ya Wizara kukubali kusafirisha Wanachama na Mashabiki wetu,zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe,".
  "Niwatakie safari njema na nina imani safari yetu ya kurudi itakuwa nzuri kwakuwa tutarudi tukiwa tayari tumeshafuzu hatua ya nusu Fainali" Rais wa Young Africans SC Eng. Hersi Said akiongea na Wanahabari wakati wa kuwaaga Wanachama na Mashabiki wanaosafiri kuelekea Afrika Kusini Makao Makuu ya Klabu Jangwani," amesema Rais wa Yanga, Hersi Said.
  Katika hatua nyingine, Rais huyo wa Yanga amezungumzia mchakato wa mabadiliko wa klabu unavyoendelea na kusema kwamba sasa itasajiliwa kampuni itakayofanya kazi na klabu anbayo itauza hisa hadi asilimia 49.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERIKALI YASAFIRISHA MASHABIKI 48 KWENDA KUISHANGILIA AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top