
WATANI wa Jadi, Simba na Yanga wametoshana nguvu kwa sare ya bila mabao katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya watani, Simba usiku huu Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha pointi 29 katika mchezo wa 11 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi moja zaidi ya JKT Tanzania ambayo pia imecheza mechi sita zaidi.
Kwa upande wao, Simba SC wanafikisha pointi 24 katika mchezo wa 11 pia, ingawa wanabaki nafasi ya tatu.
Simba SC wameondoka uwanjani wakimlalamikia refa Msaidizi namba moja, Kassim Mpanga kukataa bao lililofungwa na mshambuliaji Suleiman Abdallah Mwalimu kipindi cha pili kwa kumhukumu alikuwa ameotea.
Nao Yanga walimlalamikia Mpanga pia kipindi cha kwanza kwa kumuinulia kibendera cha kuotea mshambuliaji wao Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo akiwa anakwenda kufunga baada ya kuwazidi mbio mabeki wa Simba.
Mapema kipindi cha kwanza Yanga ilipata pigo baada ya beki wake, Dickson Job kushindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nahodha, Bakari Nondo Mwamnyeto dakika ya 38.


.png)
0 comments:
Post a Comment