• HABARI MPYA

  Sunday, February 25, 2024

  RAIS SAMIA AWAPONGEZA YANGA KUTINGA ROBÓ FAINALI LIGI YA MABINGWA


  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameipongeza klabu ya Yanga kwa kufuzu Robó Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad jana.
  “Naipongeza Klabu ya Yanga kwa kufanya vyema katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na kufanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali,”.
  “Mafanikio haya yameandika historia kubwa kwa klabu na sekta ya michezo nchini. Mmeleta furaha kwa mamilioni ya mashabiki wenu na Watanzania kwa ujumla,” amesema Rais, Dk. Samia mapema leo.
  Yanga SC jana walikata tiketi ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Yanga yalifungwa na viungo, mzawa Mudathir Yahya Abbas ‘Zanzíbar Greatest’ dakika ya 43 na Mburkinabe, Stephane Aziz Ki dakika ya 47 na washambuliaji, Mzambia Kennedy Musonda dakika ya 48 na Muivory Coast, Joseph Guede Gnadou dakika ya 84.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na Kocha Muargentina, Miguel Ángel Gamondi inafikisha pointi nane na kusogea nafasi ya pili, nyuma ya mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri baada ya wote kucheza mechi tano, wakati CR Belouizdad wanabaki na pointi zao tano, mbele ya Medeama SC ya Ghana yenye pointi nne inayoshika mkia baada ya wote kucheza mechi tano pia.
  Matokeo haya yanamaanisha Yanga imejihakikishia tiketi ya Robo Fainali kabla ya mechi za mwisho Machi 1 hata CR Belouizdad wakishinda dhidi ya Medeama SC kwa idadi ya kubwa mabao.
  Kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinasema timu zikilingana kwa pointi mshindi ataamuliwa kwa motokeo ya jumla baina yao na inakumbukwa CR Belouizdad ilishinda 3-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa kwanza Novemba 24 mwaka jana Jijini Algiers.
  Machi 1 Yanga watakuwa wageni wa Al Ahly Uwanja wa Cairo International, Cairo nchini Misri na CR Belouizdad watakuwa wenyeji wa Medeama Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers nchini Algeria zote zikianza Saa 1:00 usiku.
  Hii inakuwa mara ya nne Yanga kufika hatua ya Robó Fainali ya michuano hiyo, awali 1969 na 1970 mara zote wakitolewa na Asante Kotoko ya Ghana na 1998 wakati huo ikichezwa kwa mfumo wa makundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS SAMIA AWAPONGEZA YANGA KUTINGA ROBÓ FAINALI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top