• HABARI MPYA

  Thursday, February 08, 2024

  NI NIGERIA NA IVORY COAST FAINALI AFCON JUMAPILI ABIDJAN


  WENYEJI, Ivory Coast na Nigeria wamefanikiwa kutinga Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuzitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Afrika Kusini katika mechi za Nusu Fainali jana.
  Ilianza Nigeria kuitupa nje Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Bouaké.
  Beki wa PAOK ya Ugiriki, William Paul Troost-Ekong alianza kuifungia Nigeria kwa penalti dakika ya 67, kabla ya kiungo wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Teboho Mokoena kuisawazishia Bafana Bafana dakika ya 90.
  Katika mikwaju ya penalti kipa Stanley Bobo Nwabali wa Chippa United ya Afrika Kusini aliibukia shujaa kwa kuokoa mikwaju ya Mokoena na Evidence Makgopa, huku za Mihlali Mayambela na Mothobi Mvala pekee zikimpita.
  Waliofunga penalti za Nigeria ni Teremas Moffi, Kenneth Omeruo, Troost-Ekong na Kelechi Ịheanachọ, huku Temitayo Aina pekee akikosa.


  Baadaye Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara Jijini Abidjan, bao la mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Sébastien Haller dakika ya 65 likatosha kuwapeleka wenyeji, Ivory Coast Fainali wakiichapa DRC 1-0.
  Sasa Ivory Coast itakutana na Nigeria katika ‘Bonge la Fainali’ Jumapili Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny Jijini Abidjan yakiwa ni marudio ya mchezo wa Kundi A mwanzoni mwa mashindano Super Eagle ikiwatandika Tembo 1-0.
  Afrika Kusini na DRC zitacheza mechi ya kuwania nafasi ya tatu Jumamosi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI NIGERIA NA IVORY COAST FAINALI AFCON JUMAPILI ABIDJAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top