• HABARI MPYA

  Tuesday, December 19, 2023

  ONANA APIGA ZOTE MBILI SIMBA SC YAITANDIKA WYDAD 2-0 DAR


  WENYEJI, Simba SC wamefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad Club Athletic ya Morocco katika mchezo wa Kundi B leo Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Pongezi kwa mfungaji wa mabao yote hayo, kiungo mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana (23) aliyemtungua kipa mkongwe wa Morocco, Youssef El Motie dakika ya 36 na 38.
  Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi tano katika mchezo wa nne na kupanda nafasi ya pili nyuma ya vinara, ASEC Mimosas wenye pointi saba za mechi tatu.
  Wydad Club Athletic inarudi mkiani ikibaki na pointi zake tatu za mechi nne, nyuma ya Jwaneng Galaxy ya Botswana yenye pointi nne za mechi tatu.
  Mchezo wa Kundi B utafuatia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny Jijini Abidjan baina ya wenyeji, ASEC Mimosas na Jwaneng Galaxy.
  Mechi zijazo, Simba SC watakuwa wageni wa ASEC Mimosas Februari 23 Jijini Abidjan, kabla ya kuwakaribisha Jwaneng Galaxy Machi 1, mwakani kukamilisha Hatua ya makundi na kuangalia mustakabali wake wa kwenda Robo Fainali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ONANA APIGA ZOTE MBILI SIMBA SC YAITANDIKA WYDAD 2-0 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top