• HABARI MPYA

  Saturday, June 25, 2022

  YANGA SC YAENDELEZA REKODI YA KUTOPOTEZA MECHI LIGI KUU


  MABINGWA, Yanga wameendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi msimu huu baada ya kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.  
  Mshambuliaji Mkongo, Heritier Makambo alianza kuifungia Yanga dakika ya 40, kabla ya kiungo Mganda, Joseph Ssemunju kuisawazishia Mbeya City kwa penalti dakika ya 50 kufuatia Nahodha, Bakari Mwamnyeto kuunawa mpira kwenye boksi.
  Yanga wanafikisha mechi 29 bila kupoteza mechi, wakiwa tayari mabingwa kwa pointi zao 71, nyuma yao wakiwa mabingwa wa misimu minne iliyopita, Simba SC wenye pointi 60 za mechi 28 na kesho watamenyana na Tanzania Prisons hapo hapo Sokoine, Mbeya.
  Kwa Mbeya City, sare hiyo inawafanya wafikishe pointi 39 baada ya mechi 29 katika nafasi ya tisa.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Kagera Sugar wameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Coastal Union bao pekee la beki David Luhende dakika ya 15 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Nayo imeichapa Polisi Tanzania 1-0, bao pekee la Raymond Masota dakika ya nane Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
  Uwanja wa Karume, mjini Musoma mkoani Mara, Biashara United imeshinda 1-0 dhidi ya KMC bao pekee la Gerson Kabeja dakika ya 45 na ushei.
  Na Uwanja wa Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma, Ruvu Shooting imeichapa Mbeya Kwanza mabao 2-1.
  Mabao ya Ruvu Shooting yamefungwa na Rashid Juma dakika ya 50 na Fullu Zulu Maganga dakika ya 66, wakati la Mbeya Kwanza limefungwa na Oscar Mwajanga dakika ya 78.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEZA REKODI YA KUTOPOTEZA MECHI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top