• HABARI MPYA

    Tuesday, June 07, 2022

    SERENGETI GIRLS WAPEWA HESHIMA YA KIPEKEE BUNGENI


    TIMU ya taifa ya wanawake ya soka chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) imeweka  historia  ya kuwa  timu ya  kwanza kupewa heshima na Bunge la Jamhuri ya Muungano kuingia  na kukaa kwenye viti vya mawaziri ndani ya bunge  baada ya kufuzu kuingia  mashindano ya dunia ikiwa ni heshima ya mashujaa wa Taifa kwa kazi kubwa iliyoifanya ambapo kesho ni zamu ya Timu ya soka ya Taifa ya Walemavu ya (Tembo Warriors) ambayo pia imefuzu  mashindano ya dunia ya soka kwa walemavu.
    Akiongea  mara baada ya kuketi eneo hilo rasmi la mawaziri, Waziri mwenye dhamana ya Michezo nchini. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema ushindi huo unatokana  na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuiwezesha  timu hiyo katika kipindi chote cha  maandalizi wa  mashindano hayo.
    “Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha, kututia moyo na kutufuatilia kwa karibu sana katika kipindi chote” amefafanua Mhe. Mchengerwa.





    Aidha, amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuisaidia timu hiyo ili iweze kwenda  na kushinda kwenye mashindano hayo hatimaye kurejesha kombe hilo  la dunia na kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kuwatia moyo  na kuwasaidia ili washinde.
    Akizungumzia jinsi  timu ilivyopambana hadi kufika hapo amesema  kuwa  timu ilianza kuchabanga  Botswana magoli 11-0, ikaitandika  Burundi jumla ya magoli 6-1, na ikamalizia na kuibamiza timu ya Cameroon jumla ya magoli 5-1.
    Kwa upande wa Warriors amesema iliishindilia Cameroon mabao 5-0, kabla ya kuikandamiza Senegal goli 1-0 na kuichakaza Morroco magoli 2-0.
    Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kufanya mapinduzi makubwa katika sekta za michezo na Sanaa ili kuipeleka Tanzania kimataifa ambapo amefafanua kuwa kuanzia Februari mwaka huu timu zote za taifa zinazoshiriki kwenya mashindano ya kimataifa  zimewekwa kambini na zinagharimiwa na Serikali.
    Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo Noela Luhala alipewa heshima ya kuzungumza mbele ya Bunge tukufu ambapo ameishukuru Serikali na Bunge kwa mchango iliyowapa. @serengetigirlstz
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERENGETI GIRLS WAPEWA HESHIMA YA KIPEKEE BUNGENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top