• HABARI MPYA

    Sunday, June 27, 2021

    WANACHAMA WA YANGA WAPITISHA MABADILIKO YA KATIBA KUELEKEA MFUMO MPYA WA UENDESHAJI KLABU YAO

    WANACHAMA wa klabu ya Yanga kwa kauli moja leo wamepitisha Mabadiliko ya Katiba yatakayowawezesha kufanya marekebisho ya mfumo wa uendeshaji.
    Wanachama hao wameunga mkono mabadiliko hayo katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa DYCC, Chang’ombe Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais mstaafu wa awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi.
    Katika mkutano huo, Rais Mstaafu Jakaya ambaye pia ni mwanachama wa klabu hiyo, alimsifu Mwenyekiti, Dk. Mshindo Mbette Msolla kuiongoza vyema klabu hiyo.


    Mzee Kikwete pia akaitilia ubani klabu kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya watani Jumamosi kwa kusema; "Yanga ni timu yangu, naipenda sana, inapofungwa naumia inaposhinda nafurahi sana na naamini Jumamosi ijayo tutashinda,".
    Aidha, Dk Msolla, kocha wa zamani wa timu ya taifa na klabu mbalimbali alitangaza Baraza jipya la Wadhamini wa klabu ambalo litaundwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Huruma Mkuchika, Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge Tarimba Gulam Abbas na Mama Fatma Karume ambaye ni mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amaan Karume.
    Dk Msolla pia amesema katika kuzingatia kuleta umoja ndani ya klabu, Wajumbe watatu waliokuwa wamesimamishwa mwaka jana, Said Rupia, Rodgers Gumbo na Frank Kamugisha wamerudishwa kwenye nafasi zao kuendelea kwenye majukumu yao.
    Aidha, Katibu Kamati ya Ujenzi, Mhandisi Said Mrisho aliwasilisha Mwonekano wa mradi wa ujenzi wa Viwanja vya Mazoezi na hosteli utakaofanyika kwenye eneo la timu huko Kigamboni, Dar es Salaam utakavyokuwa baada ya kumalizika.
    Kwenye majengo haya kutakuwa na Viwanja viwili vya mazoezi, Uwanja wa nyasi bandia na nyasi za kawaida, hosteli za kisasa za wachezaji pamoja na benchi la ufundi, bwawa kubwa na la kisasa la kuogelea na maeneo mengine ya kisasa ya kufanyia mazoezi na kituo cha mazoezi kikubwa na cha kisasa kuwahi kutengenezwa nchini.
    Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau ambaye aliunga mkono mabadiliko hayo na kuahidi kuwa bega kwa bega na klabu hiyo.
    Kwa upande wake, Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Azam Media Limited, Yahya Mohamed ameahidi kuendeleza ushirikiano baina yao na klabu hiyo kubwa nchini.
    Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji ameunga mkono mabadiliko hayo na kusema ataangalia namna ya kushiriki baadaye.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANACHAMA WA YANGA WAPITISHA MABADILIKO YA KATIBA KUELEKEA MFUMO MPYA WA UENDESHAJI KLABU YAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top