• HABARI MPYA

    Tuesday, May 25, 2021

    AZAM TV WAINGIA MKATABA MPYA MNONO NA TFF SHILINGI BILIONI 225.6 KURUSHA MECHI ZA LIGI KUU YA TANZANIA BARA MIAKA 10

    KAMPUNI ya Azam Media Limited imeingia mkataba mpya wa haki za matangazo ya Televisheni katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Mkataba huo wa miaka 10 kuanzia msimu ujao umesainiwa leo hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam na una thamani ya Sh. Bilioni 265.
    Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Muhando  amesema kwamba thamani ya mkataba huo imetokana na uzoefu wa miaka minane katika kurusha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ambako walijifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuona jinsi timu zinavyojiendesha na changamoto zake.
    “Miaka minane iliyopita, imetufanya kufahamu uendeshaji wa timu, tumeona changamoto nyingi wanazopitia, tumeona maisha ya wachezaji na tumekuwa sehemu ya maisha hayo ndio maana tumeguswa kwa kiasi kikubwa katika mkataba huu.

    Hilo limetufanya tuongeze kiwango cha fedha cha udhamini wa kuonyesha matangazo ya ligi hiyo kwa sababu ni ukweli kuwa tunafanya biashara, lakini hii ya kwetu ni biashara ya kizalendo.
    Thamani hiyo ya mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 225. 6 itakuwa na manufaa si katika soka tu, ila pia kwa Serikali ambayo itanufaika na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwani Azam Media Limited tutalipa kiasi cha Shilingi bilioni 34.4.
    Sisi Azam Media Limited tunataka kuongeza hamasa ya burudani na kuufanya mpira wa miguu wa Tanzania kuwa katika kiwango cha kimataifa na weledi zaidi.
    Tunaamini mashabiki wa mpira wa miguu nchini wamefurahia kazi yetu ambayo tuliifanya kwa miaka minane iliyopita. Matangazo hayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kipindi hicho yametupa uzoefu mkubwa na mafanikio tuliyoyapata yametupa hamasa kuendelea tena.
    Miaka minane imetupa uzoefu wa kutosha, ahadi yetu ni kuwa miaka kumi ijayo tutafanya mambo makubwa zaidi kwa kurusha matangazo yenye ubora wa kimataifa kama ilivyo katika nchi zilizoendelea. Kwa kutambua hilo tumeimarisha studio zetu kwa kuongeza vifaa vya kisasa na kuimarisha mitambo, vyote hivyo vitafanya matangazo yetu kuwa katika ubora wa kiwango cha juu zaidi.
    Katika mkataba huu mpya, tunaahidi kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu Bara kwa asilimia 100, kwani hata ligi iliyopita mathalani msimu huu unaokaribia kumalizika, tumeonyesha asilimia 99 ya mechi zote, zile chache ambacho hatukuonyesha haikuwa kwa sababu ya Azam Media Limited, ilikuwa changamoto nje ya uwezo wetu.
    Tunaamini kwa kuonyesha mechi zote itasaidia timu kupata wadhamini binafsi, pia itawasaidia wachezaji kujitangaza zaidi ndani na nje ya nchi hivyo kupandisha thamani yao bila kusahau kuwa itafanya waamuzi wachezeshe kwa weledi zaidi.
    Katika mkataba huu ambao umeboreshwa zaidi na zaidi, timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara zitanufaika kwa kiwango kikubwa na tunaamini kuwa kutakuwa na ushindani wa hali ya juu na ligi yetu itakuwa bora zaidi Afrika.
    Hatuna shaka kuwa mkataba huu unaweza kuwa miongoni mwa mikataba mikubwa na yenye kiasi kikubwa cha fedha Kusini mwa Jangwa la Sahara katika mikataba ya matangazo ya mpira na maendeleo ya soka.
    Ikumbukwe kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako mechi zote za Ligi Kuu zinaonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni tena bila kubagua timu ndogo wala kubwa. Nchi nyingine huonyesha mechi chache tu tena za klabu kubwa. Kazi hiyo inaweza kufanywa na Azam Media Limited tu.
    Dira yetu siku zote imekuwa ni kujenga na kuifanya Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa miongoni mwa ligi tano bora katika bara la Afrika. Mkataba huu ambao tumeusaini leo umeonyesha njia jinsi ya kufikia katika malengo hayo. Hilo tunaliahidi kulifanya kwa juhudi na nguvu zetu zote kwa kushirikiana na wadau wote wa soka nchini.
    Thamani ya mkataba huu ni kubwa sana, sisi Azam hatukujali gharama za uzalishaji ambazo huhitaji wafanyakazi wengi viwanjani, gharama za satellite, vifaa vya kurushia matangazo na mambo mengine mengi yanayohusu matangazo ya moja kwa moja.
    Ushiriki na thamani ya mkataba huu ni kwa ajili ya maendeleo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kwa kutambua hilo, fedha ambayo imewekezwa katika mkataba huu, asilimia 67 itakwenda moja kwa moja kwa timu ambazo zinashiriki ligi hiyo.
    Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa kwa msimu ujao yaani 2021/2022, Azam Media Limited itatoa Shilingi bilioni 12, huku timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara zikipata Shilingi bilioni nane, mgao mwingine utakwenda kwa maendeleo ya soka, TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).
    Fedha hizo zitaendelea kuongezeka kwa kila msimu na msimu wa mwisho wa mkataba yaani 2030/2031, Azam itatoa Shilingi bilioni 28 na wakati huo timu zote kwa ujumla zitapata takribani Shilingi bilioni 19. 
    Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa ndani ya miaka kumi, kiwango ambacho kitatolewa msimu ujao kitaongezeka zaidi ya mara mbili mpaka itakapofika msimu wa mwisho wa mkataba.
    Ili kuifanya timu yetu iwe na ushindani zaidi, kila nafasi ambayo timu imemaliza katika Ligi Kuu Tanzania Bara itakuwa na bonasi ambayo itatolewa kulingana na nafasi ya timu kwenye msimamo wa ligi.
    Mathalani, kwa msimu mitatu ijayo yaani 2021/22 mpaka 2023/24, bingwa wa Tanzania Bara atakuwa akipata Shilingi milioni 500 kwa msimu. Mshindi wa pili Shilingi milioni 250, mshindi wa tatu Shilingi milioni 225 na mshindi wa nne Shilingi milioni 200. 
    Fedha hizo zitakuwa zikiongezeka kila msimu na ndio maana msimu wa 2028/29 mpaka 2030/31 bingwa atakuwa akipata Shilingi milioni 700 kwa msimu. Mshindi wa pili Shilingi milioni 325, mshindi wa tatu Shilingi milioni 275 na mshindi wa nne Shilingi milioni 250.
    Tunaamini kuwa timu hizo nne ndio zitakazokuwa zinashiriki michuano ya kimataifa (kutokana na nafasi zinazotolewa na CAF) kwa hiyo zinahitaji maandalizi mazuri ikiwa ni pamoja na kufanya usajili mzuri, kuweka kambi nzuri, kusafiri na mambo mengine yanayohusu maandalizi ya mashindano hayo.
    Bonasi hizo hazitaishia kwa timu nne za juu tu, kila nafasi kutakuwa na bonasi yake, kwa msimu mitatu ya kwanza 2021/22 mpaka 2023/24 na misimu mitatu ya mwisho 2028/29 mpaka 2030/31, bonasi zitatolewa kama ifuatavyo;


    Pia zawadi hizi zitaongezeka kila msimu katika kipindi cha miaka yote kumi ya mkataba huu.
    Kama hiyo haitoshi, tumefanya uchunguzi wetu wenyewe tukagundua kuwa ili timu ziweze kusafiri vizuri wakati wa ligi, kulipa wachezaji wake mishahara na kuweka kambi nzuri zinahitaji kuwa na fedha na kwa kuangalia hilo katika kipindi cha miezi kumi ya ligi kila msimu tutakuwa tunatoa bonasi kwa kila timu.
    Kwa msimu wa 2021/22 mpaka 2023/24 mgao kwa kila timu kwa kila mwezi utakuwa kati ya Shilingi milioni 40 mpaka milioni 50 na kiwango hicho kitakuwa kinaongezeka kila baada ya kipindi fulani.
    Kiwango hicho kitapanda kila mara mpaka mwisho wa mkataba huu utakapoisha miaka kumi ijayo. Msimu wa 2028/29 mpaka 2030/31 kila timu itakuwa inapata bonasi ya Shilingi milioni 82 mpaka Shilingi milioni 102. Fedha hizi zitatolewa kwa mpangilio maalumu ili kuzuia zisitumike nje ya maandalizi ya timu na maendeleo ya soka.   
    Sisi Azam Media Limited, tunaamini kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na wadau wengine kama Bodi ya Ligi (TPLB) na Serikali watatupa ushirikiano wa kutosha ili kukamilisha nia yetu hii nzuri ya kuendeleza mpira wa miguu nchini.
    Hayo yatawezekana kama kutakuwa na kanuni za soka za Ligi Kuu Tanzania Bara zenye viwango na zinazojitosheleza na ambazo zitarahisisha malengo yetu yaani sisi AML kuifanya ligi yetu kuwa miongoni mwa ligi bora Afrika.
    Utashi wa kisiasa, ushirikiano kutoka serikalini bila kusahau vyombo vya habari vya ndani utafanya malengo yetu yatimizwe kwa haraka zaidi.
    Ili kuifanya ligi yetu iendeshwe kisasa zaidi, tungeshauri kusiwe na maamuzi yanayofanywa kisiasa ambayo yanaweza kusababisha  kuongezwa kwa timu kwani hilo litasababisha kuvurugwa kwa ratiba na bajeti ambayo tayari imezingatia idadi ya timu zilizopo.
    Tumekubaliana na TFF kwamba wanakwenda kuwekeza zaidi katika mfumo wa kutumia fedha mtandaoni ambao utasaidia udhibiti wa fedha. Mfumo huu utasaidia kudhibiti matumizi ya kila mwezi na ni lazima utumiwe na klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara watakapokuwa wanafanya maombi ya fedha, matumizi na marejesho. 
    Lengo la mfumo huu ni kuongeza uwazi na kuhakikisha kuwa fedha zote zinatumika katika uendeshaji wa Ligi Kuu Bara. Timu zikiwa na mifumo imara ya fedha zitakuwa na uwezo wa kujiendesha na kushindana kimataifa.
    Katika mkataba huu, malipo yote kwa klabu yatafanywa kwa miezi kumi wakati wa ligi, lakini yatalipwa sawa kila mwezi. Lengo ni kudhibiti na kuzuia matumizi ambayo hayamo katika mkataba huu.  
    Tungependa kuona wadau wa soka wakiwemo mashabiki wa soka, waandishi wa habari, TFF, TPLB na taasisi nyingine za Serikali kama TRA, wakishiriki kupiga vita na kuondoa ukiukwaji wa haki za matangazo ya mpira na hasa mitandaoni au kupitia kwenye televisheni za ‘cable’.
    Sisi Azam Media Limited (AML) tunaahidi kuwa tunakwenda kuongeza ubora katika matangazo yetu na ndio maana tumeazimia kuweka taa katika viwanja vingine vinne ili kuwezesha mechi nyingi zaidi kuchezwa usiku na kuongeza burudani. Hili linaweza kuongezeka kutokana na mazingira yatakavyokuwa yanaruhusu.
    Tumeanza utekelezji wa hilo katika Uwanja wa Majaliwa na tunafuatilia mchuano wa timu ambazo zitashuka daraja ili kujua viwanja vingine vitatu ambako tutafunga taa.
    Kwa ujumla miaka kumi ijayo, tunaamini itakuwa ni ya kipekee kwa Watanzania, itakuwa zaidi ya burudani na hakika hakuna atakayejuta kwani tumejipanga vya kutosha.  Uwezo wetu wa kuonyesha mechi umeongezeka na sasa tunaweza kuonyesha mechi zote za msimu. Tunawashukuru sana, tunaomba ushirikiano wa wadau wote wa soka,”amesema Tido Mhando, Ofisa Mtendaji Mkuu Azam Media Limited. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM TV WAINGIA MKATABA MPYA MNONO NA TFF SHILINGI BILIONI 225.6 KURUSHA MECHI ZA LIGI KUU YA TANZANIA BARA MIAKA 10 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top