• HABARI MPYA

    Wednesday, July 11, 2018

    NANI ANAWEZA KUDHIHIRISHA NI YANGA KULIKO TARIMBA ABBAS?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    HALI si shwari Yanga, baada ya Mwenyekiti wa Kamati maalumu ya kusimamia shughuli za uendeshwaji wa klabu hiyo, Tarimba Abbas kujiuzulu juzi akidai kuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Clement Sanga ni tatizo.
    Siku moja baada ya hatua hiyo, jana imetoka taarifa ambayo licha ya kuwa na saini ya mtu mmoja ambaye hata hivyo, hakubainisha jina wala wadhifa wake ikisema viongozi wa matawi ya klabu ya Yanga wanamuunga mkono Sanga na wanamuona Tarimba kama msaliti na adui wa klabu hiyo.
    Juni 10 mwaka huu, katika Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga waliunda kamati ya watu tisa chini ya Tarimba ambaye aliwahi kuwa Rais wa klabu hiyo, kusimamia shughuli mbalimbali za klabu hiyo baada ya kile kilichoonekana kuelemewa kwa uongozi uliopo madarakani chini ya Sanga.

    Tarimba Abbas amejiuzulu Uenyekiti wa Kamati maalumu ya kusimamia shughuli za uendeshwaji wa klabu ya Yanga

    Katika kamati hiyo, Tarimba alikuwa anasaidiwa na Saidi Mecky Sadiki ambaye ni makamu mwenyekiti na wajumbe, Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majid Suleiman na Hussein Ndama.
    Tangu kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji, kamati ya utendaji ya klabu hiyo imemomonyoka kutokana na wajumbe wake wengi ambao walichaguliwa Juni, 2016 pia kuchukua uamuzi huo. Walioungana na Manji kujiweka kando katika uongozi wa Yanga ni Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah. Waliobaki pamoja na Sanga ni wanne tu ambao ni, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    Doa la kwanza katika kamati ya Tarimba lilianza tangu Juni 10 ilipotangazwa baada ya mjumbe mmoja, Abdallah Bin Kleb kukataa uteuzi huo akisema anakabiliwa na matatizo ya kiafya na pia amebanwa na majukumu yake mengine ya biashara zake.
    Wakati Bin Kleb akisema hayo, kuna taarifa nyuma ya pazia ambazo zinadai kwamba Sanga amegoma kufanya kazi na kamati hiyo. Mara tu baada ya kuundwa, kulikuwa na madai kwamba haitaki na kwamba alikuwa akiipiga vita. Baadaye Sanga akaibuka na kusema kwamba shughuli za klabu hiyo zitaendelea kufanywa na uongozi wake na kamati zake alizounda na kwamba kamati ya Tarimba itakuwa ya ushauri na misaada ya kifedha pekee.
    Pamoja na msimamo huo wa kaimu mwenyekiti, bado Tarimba aliendelea kufanya kazi na alikaririwa na vyombo vya habari akisema ataongoza usajili wa wachezaji kimyakimya wakishirikiana na kamati ya utendaji.
    Sakata hilo lilikolea mwishoni mwa wiki baada ya Sanga kukutana na viongozi wa matawi na kuiponda kamati ya Tarimba huku akisema kwamba Manji ameomba miezi mitatu kabla ya kurejea kuendelea na majukumu yake klabuni.
    Katika mkutano wa Juni 10, licha ya wanachama wa Yanga kuunda Kamati ya Tarimba, walikataa ombi la Manji la Mei mwaka jana la kujiuzulu na kusema bado wanamtambua kama kiongozi wao mkuu na baada ya kikao cha Jumapili, haikuwa ajabu jana usiku kumsikia Tarimba kupitia kituo cha Redio Uhuru akitangaza kujiuzulu hiyo ikiwa na maana kwamba hata kamati yake nayo haipo tena licha ya kuundwa na wanachama baada ya kuchoshwa na mwenendo wa klabu chini ya Sanga baada ya Manji kujiondoa.
    Kufa kwa kamati hiyo ya Tarimba ikiwa ni moja ya mambo yaliyoazimiwa katika mkutano kunafanya kubaki kwa azimio lingine moja ambalo lilitangazwa siku hiyo ya mkutano na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyekuwa mgeni rasmi. Aliwapa viongozi wa Yanga miezi mitatu kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu, akiwamo Manji.
    Baada ya agizo la Dk. Mwakyembe, waandishi wa habari waliondolewa kwenye ukumbi wa mkutano ili yote yaliyokuwa yanajadiliwa yawe siri, ingawa baada ya mkutano huo wadadisi walidodosa na kupata undani wa yaliyojiri na kujadiliwa. Kwa bahati nzuri, Yanga yenyewe kupitia kwa katibu mkuu wake, Charles Boniface Mkwasa ikatangaza kuundwa kwa kamati ya Tarimba na kuahidi kufanyia kazi agizo la Waziri kwa kuitisha uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za wajumbe waliojiuzulu.
    Baada ya mwezi mmoja tu, imekuwa tafrani Yanga – hakuna Kamati ya Tarimba wala mwito wa uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za wajumbe waliojiuzulu na zaidi kiza ni kinene juu ya mustakabali wa klabu. Wanachama, au viongozi wa matawi kumuita Tarimba msaliti wa Yanga inataka moyo mno, kwa sababu huyo ni mpenzi kweli klabu hiyo ambaye tangu angali kijana mdogo amekuwa akijitolea kwa hali na mali juu ya ustawi wa klabu. Tarimba ameanza kuitumikia Yanga akiwa kijana mdogo mwenye nguvu miaka ya 1980 na akarejea miaka ya 1990 hadi 2000 mwanzoni. 
    Alipumzika, baada ya kufanya kazi kubwa ya kutengeneza muundo mpya wa uendeshwaji wa klabu hiyo kwa kuingiza wasomi zaidi na watu wenye uwezo wa kifedha, ili kuiondoa klabu kwenye zama za kuongozwa na watu wasiokuwa nguvu wala ushawishi wa kifedha.
    Huo ndiyo ukawa mwanzo wa Yanga kupata viongozi kama Francis Mponjoli Kifukwe, mawakili Imani Madega, Lloyd Nchunga na sasa Manji, Sanga na wengine. Baada ya Manji kujiuzulu Mei mwaka jana, klabu ikawa na hali ngumu mno kifedha, lakini Tarimba akiwa bosi mkubwa wa kampuni ya SportPesa, Yanga ikapata udhamini wa kampuni hiyo ya michezo ya kubahatisha. 
    Kwa kuwakumbusha tu wanaombeza na kumkashifu Tarimba, huyo ndiye kiongozi wa kwanza kuipatia Yanga udhamini rasmi, kwanza wa kampuni ya simu za mkononi, Tigo na baadaye Shivacom, waliokuwa wakala wa kampuni ya simu ya Vodacom. 
    Unaweza kutilia shaka Uyanga wa hao viongozi wa matawi na Kaimu Mwenyekiti, Sanga na watu wake wote akina Nyika, Lukumay na Dismas Ten – lakini si Uyanga wa Tarimba. Tarimba ni Yanga lialia. Wakati wa ujana wake, Tarimba alikuwa tayari kugombana na mtu yeyote kwa ajili ya Yanga. 
    Machi 31, mwaka 2002 Yanga ilifungwa mabao 4-1 na Simba katika fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Tusker Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Tarimba akiwa mwenyekiti. Mechi hiyo iliyohudhuriwa na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya mshambuliaji wa Simba, Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. 
    Tarimba aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Mwamuzi wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo, wakati Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT) chini ya Mwenyekiti, Muhiddin Ahmed Ndolanga na Katibu wake, Alhaj Ismail Aden Rage wakamfungia Tarimba mwaka mzima na hata alipomaliza adhabu yake, hakurejea kuongoza hadi anaibuka tena kwenye Kamati iliyoundwa Juni 10. 
    Inataka moyo sana kumuita Tarimba msaliti na asiyeitakia mema Yanga. Akiwa mfanyabiashara, mtumishi mstaafu wa muda mrefu wa taasisi ya umma na kwa sasa bosi mkubwa wa Sport Pesa, Tarimba ana shida gani zaidi ya mapenzi tu kwa Yanga? Tuamini tunavyoaminishwa na wafuasi wa Sanga kwamba Tarimba ni adui wa Yanga – basi sasa tuambiwe ni nini mustakabali wa klabu.
    Pamoja na fedha za SportPesa wachezaji wanagoma kila mwezi sababu ya mishahara, huduma mbovu na hata matokeo mabaya ya msimu uliopita yametokana na hali halisi ya klabu kuwa mbaya. Zaidi ya hapo kuna dalili za ubadhirifu ndani ya klabu, kwamba Yanga ina hali ngumu lakini pia kuna wasiwasi hicho kidogo kinachopatikana kinaliwa na wajanja na wachezaji wanaendelea kupiga miayo. 
    Tarimba hawezi kumpinga Manji. Wala mwana Yanga yeyote mwenye kuitakia mema klabu hawezi kumpiga Manji bali, watu wanaumizwa na hali halisi ndani ya klabu.
    Imefikia wapenzi wanachama wa Yanga wanaona kama Sanga anajali zaidi masilahi yake binafsi na anataka kuhakikisha anaendelea kuwa kiongozi mkuu wa klabu ili abaki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kwa masilahi yake zaidi. 
    Manji ainuke aseme neno kuwatuliza wana Yanga na waanze kumuamini tena Sanga. Lakini mapambano baina ya wana Yanga kwa wana Yanga ya nini? Kuna usemi maarufu alikuwa anapenda kuutumia Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete; “Sote tunajenga nyumba moja, ya nini kugombea fito” na inawezekana ndiyo maana Tarimba amejitoa.
    Ila kati ya wanamuita msaliti, nani anaweza kuibuka kudhihirisha ni Yanga kuliko Tarimba Abbas?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NANI ANAWEZA KUDHIHIRISHA NI YANGA KULIKO TARIMBA ABBAS? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top