• HABARI MPYA

    Sunday, April 12, 2015

    YANGA SC WAO NAO NA UBINGWA PUA NA MDOMO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imezidi kupaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
    Yanga SC sasa wanafikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 21, ikiwazidi kwa pointi nane mabingwa watetezi, Azam FC walio nafasi ya pili. 
    Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
    Amissi Tambwe angekuwa wa kwanza kuwainua mashabiki wa Yanga vitini, kama si refa Mathew Akrama wa Mwanza kukataa bao lake safi dakika ya sita, alilofunga akiwa amedhibitiwa na kipa na mabeki wa Mbeya City kwa kupiga kichwa cha kudundisha.
    Salum Telela akiwa amebebwa na wenzake baada ya kufunga bao la pili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Mbeya City leo
    Kpah Sherman wa Yanga akitafuta maarifa ya kumtoka beki wa Mbeya City, Christian Sembuli 
    Simon Msuva akimtoka beki wa Mbeya City, Richard Peter 

    Kpah Sherman akaifungia bao la kwanza Yanga SC dakika ya 19 akifumua shuti la kugeuka na mpira baada ya krosi ya beki wa kushoto, Oscar Joshua.
    Salum Telela akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 37 akimalizia mpira wa adhabu wa Haruna Niyonzima, baada ya Sherman kuchezewa rafu nje kidogo ya boksi.
    Zikiwa zimesali dakika tano mchezo kuwa mapumziko, Themi Felix Buhaja akaifungia Mbeya City bao la kufutia machozi dakika ya 40, kufuatia shambulizi la kushitukiza akimalizia pasi ya Richard Peter.
    Kipindi cha pili, Yanga SC ilirudi na moto wake na kufanikiwa kupata bao la tatu baada ya dakika tano tu, kupitia kwa Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu wa Niyonzima baada ya Juma Abdul kuangushwa na Peter Mwalyanzi.
    Themi Felix alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 54 baada ya kumchezea rafu, kiungo wa Yanga SC Salum Telela, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo na kutoka nje nafasi yake ikichukuliwa na Hassan Dilunga.
    Yanga SC iliendelea kutawala mchezo huo baada ya bao hilo na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Mbeya City, lakini bahati haikuwa yao leo hii wakali wa mabao wa timu hiyo, Simon Msuva na Tambwe walioishia kukosa mabao ya wazi.
    Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Salum Telela/Hassan Dilunga dk62, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman/Mrisho Ngassa dk70 na Simon Msuva.
    Mbeya City; Hannington Kalyesebula, Richard Peter, Hassan Mwasapili, Juma Nyosso, Christian Sembuli, Kenny Ally, Paul Nonga/Mwagane Yeya dk77, Raphael Daudi/Abdallah Seif dk60, Themi Felix, Peter Mwalyanzi na Deus Kaseke/Peter Mapunda dk60.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAO NAO NA UBINGWA PUA NA MDOMO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top