• HABARI MPYA

    Thursday, July 03, 2014

    SERENGETI BOYS WAONYWA WASIHUJUMU TIMU, WAKIFANYA HIVYO WATAJIMALIZA KISOKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wa timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ wameshauriwa kukataa kujihusisha na upangaji wa matokeo katika mechi, kwani wataharibu mustakabali wa soka yao.
    Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Uchunguzi katika Michezo (ICSS), Stuart Page katika semina ya siku moja maalum kwa wachezaji hao iliyofanyika leo katika majengo ya Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. 
    Stuart Page akitoa semina kwa Serengeti Boys leo Karume 
    Stuart katikati, kulia Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi
    Wachezaji wakisikiliza kwa makini

    Page amewaambia chipukizi hao kwamba wachezaji kadhaa wamefungiwa moja kwa moja kujihusisha na soka baada ya kugundulika walijihusisha na upangaji matokeo katika mechi.
    Amesema kuna ushawishi mwingi wa upangaji matokeo na watu huwaingia wachezaji kwa mbinu mbalimbali wakijifanya mawakala wa timu au wema wenye nia nzuri.
    Page amewaasa wachezaji hao wa Serengeti kuwa makini mno na mchezo huo kwa sababu ni hatari mno kwa mustakabali wa soka yao. Amewashauri kutoa taarifa mara moja wanapofuatwa na watu wa aina hiyo.
    Amewaambia chanzo kikuu cha upangaji wa matokeo ni kamari, ambayo watu wanaocheza kwa kuwekeana madau ya kutabiri matokeo, hujirahisishia njia za kushinda kwa kwenda kuwarubuni wachezaji kwa fedha wacheze chini ya kiwango kusaliti timu zao zifungwe. 
    Semina hiyo ICSS imefanywa pia kwa klabu mbalimbali za Ulaya zikiwemo Manchester City, Real Madrid  na Bayern Munich- maana yake na wachezaji wa Serengeti wanakuwa wenye bahati kufikishiwa ujumbe huo. 
    ICSS kesho inatarajiwa kuendesha semina kama hiyo kwa wachezaji wa kituo cha Watoto wa Mitaani cha Mwanza.
    Serengeti Boys ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika, dhidi ya Afrika Kusini ‘Amajimbos’, Ijumaa ya Julai 18 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
    Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari ameshafanya mchujo wa awali wa wachezaji wa timu hiyo kutoka 39 na kubaki na 31. Timu hiyo imepiga kambi kwenye hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Karume.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERENGETI BOYS WAONYWA WASIHUJUMU TIMU, WAKIFANYA HIVYO WATAJIMALIZA KISOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top