• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 31, 2014

  WATU WANAJIPIGIA ‘HELA’ YANGA SC KAMA HAINA WENYEWE...HAINA VIONGOZI, YAANI IPO IPO TU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  JEZI za klabu maarufu za soka nchini, Simba na Yanga zinaongoza kwa mauzo miongoni mwa jezi za timu mbalimbali duniani zinazouzwa nchini- lakini angalau Simba SC wanapata Sh. Milioni 70 kwa mwaka, lakini watani wao hawapati ‘’senti tano nyekundu.
  Uongozi uliopita Simba SC uliingia mkataba na kampuni moja kuuza jezi za klabu hiyo kwa kulipa Sh. Milioni 70 kwa mwaka na wakati huo aliyekuwa Katibu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala alisema ni bora kuanza na hivyo kuliko kutopata kitu kabisa.
  Dili la nani? Jezi ya Yanga SC ikiwa dukani sambamba na jezi za timu nyingine mbalimbali duniani. Inaelezwa jezi hiyo inaongoza kununuliwa


  Kweli, Sh. Milioni 70 ni ndogo kulingana na soko la jezi za Wekundu wa Msimbazi- lakini kama kweli kwa kuanzia huku mikakati mingine ya kuchuma fedha zaidi kutokana na biashara hiyo inaendelea si mbaya.
  Vipi kuhusu watani wao, Yanga SC ambao inaelezwa jezi zao ndizo zinaongoza kununuliwa. BIN ZUBEIRY imefanya mahojiano na wafanyabiashara kadhaa wa jezi, wa jumla na rejareja ambao wamesema jezi za Simba na Yanga ni ‘dili sokoni’.
  “Hizi jezi za Simba na Yanga kwa sasa hivi zinanunuliwa kuliko hata hizo jezi za timu za Ulaya, zinanunuliwa sana,”alisema mfanyabishara mwenye duka lake Kigamboni, Dar es Salaam.
  Alipoulizwa wapi wanapata jezi hizo, alisema; “Sisi tunanunua kwenye maduka ya jumla ya Kariakoo tunakuja kuuza huku,”.
  Viongozi wa Yanga SC walikwenda kununua jezi Kariakoo ili wamvalishe Mrisho Ngassa wakati anarejea kwenye timu hiyo mwaka jana

  Hata watembezaji wengi wa jezi nao wanasema wananunua kwenye maduka ya jumla Kariakoo na wanasema ni biashara ya uhakika kwa sasa.
  “Kwa mfano kama Yanga inacheza pale tu Taifa, ukienda na jezi 100 hairudi hata moja, kwa mikoani wakati mwingine unakwenda hata na jezi 500 na hazirudi,”amesema mfanyabishara mwingine Tandika, Dar es Salaam.
  Lakini wafanyabiashara wengi hawajui kama wanauza jezi hizo kinyume cha sheria kwa sababu Yanga wenyewe hawajawahi kuchapisha jezi na hawana mkataba na mtu, au taasisi yoyote kufanya biashara hiyo.
  “Sisi tunauza tu, kitu kinauzwa kwenye maduka makubwa ya watu ambao wanalipa kodi zao nyingi serikalini, maana yake wanauza kihalali, sasa hatujui kama Yanga wanajua au hawajui,”amesema mfanyabiashara wa Kariakoo.
  Hii si biashara haramu, wapenzi wa Yanga wakununua jezi za timu yao

  Lakini kushamiri kwa biashara hiyo haramu kunachangiwa na Yanga wenyewe- kiasi kwamba inatia shaka labda kuna viongozi wanahusika kwa sababu- kwanza inafumbiwa macho iendelee katika mazingira hayo bila klabu kupata senti moja.
  Wakati mwingine, viongozi wa Yanga wenyewe wamekuwa wakienda kununua jezi hizo feki kwa ajili ya kuwavalisha wachezaji wao wapya wakati wanawasajili au kuwasili nchini.
  Bado ni kitendawili kigumu juu ya biashara hii ya jezi ndani Yanga  ambayo ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato kwa klabu kubwa Ulaya- kama kweli viongozi wa klabu hiyo hawafahamu lolote, au wanawapiga changa la macho wanachama wao?  
  Haifanani na biashara haramu kwa sababu inauzwa kiholela kama njugu kuanzia kwenye maduka makubwa, madogo hadi kwa watembezaji nchi nzima. 
  Kwa vyovyote, Yanga SC inapoteza si chini ya Sh. Milioni 500 kwa mwaka kutokana na mauzo ya jezi pekee- achilia mbali kama wangebuni bidhaa nyingine zenye nembo yao. 
  Ni kitendawili kilichokosa mteguzi kwa muda sasa juu ya ukweli wa mauzo ya jezi za Yanga. Viongozi Yanga wananunua jezi feki, wanachama na wapenzi kadhalika- nani amkataze nani, nani amlaumu nani na nani anaumia klabu kuhujumiwa kiasi hicho? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WATU WANAJIPIGIA ‘HELA’ YANGA SC KAMA HAINA WENYEWE...HAINA VIONGOZI, YAANI IPO IPO TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top