• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 24, 2014

  BREAKING NEWS; YANGA YAJITOA KOMBE LA KAGAME

  Na Samira Said, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imejitoa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame) kwa madai kuwa hadi sasa haijapewa barua ya kualikwa kushiriki.
  Katibu wa Yanga SC, Benno Njovu ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba hawajapata mwaliko wowote rasmi kutoka Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), waandaaji wa michuano hiyo. 
   “Yanga haijapata mwaliko wowote kuhusu mashindano ya Kombe la Kagame kutoka CECAFA,” amesema.
  Lakini katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRYA kwamba wamekuwa wakiitarifu klabu hiyo mara kwa mara kadiri wanavyopata taarifa kutoka CECAFA. 
  Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mbrazil Marcio Maximo (kushoto) ameitoa timu hiyo kwenye Kombe la Kagame 

  Pamoja na Njovu kusema kwamba hawana taarifa za mashindano, lakini BIN ZUBEIRY inafahamu kocha wao Mkuu, Mbrazil, Marcio Maximo ndiye ameitoa timu hiyo kwenye mashindano hayo.
  Maximo amesema kwamba kikosi chake bado hakijawa tayari kushiriki mashindano ndani ya wiki mbili au tatu, na ametaka muda zaidi wa maandalizi.
  “Maximo amesema sehemu kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza wapo Taifa Stars, na tangu amekuja nchini hajawahi kufanya nao mazoezi. Wachezaji wengine Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza wapo na timu yao ya taifa ya Uganda na Haruna Niyonzima yupo na timu yake ya taifa ya Rwanda.
  Anatarajia kuwapata wachezaji wa timu za taifa kuanzia Agosti 5 na wakati Kagame inaanza Agosti 8, hawezi kupata muda wa kutosha wa kuwaunganisha na wenzao, hivyo ameomba muda zaidi wa kuiandaa timu,”kimesema chanzo kutoka Yanga.
  Vijana hawako tayari kwa mashindano

  Imeelezwa Maximo amependekeza timu ya vijana, Yanga B ndiyo iende kwenye mashindano hayo, lakini yeye apate fursa ya kuandaa kikosi kwa ajili ya Ligi Kuu. 
  Yanga SC imepangwa Kundi A pamoja na wenyeji Rayon Sport, KMKM ya Zanzibar, Atlabara ya Sudan Kusini na Coffee ya Ethiopia. Imepangiwa kufungua dimba na wenyeji Rayon Sport Uwanja wa Amahoro, Kigali nchini Rwanda Agosti 8, mwaka huu, kabla ya kucheza na KMKM, Agosti 10, Atlabara Agosti 12 na Coffee Agosti 16.
  Yanga SC inayofundishwa Marcio Maximo anayesaidiwa Leonardo Neiva, wote Wabrazil na mzalendo Salvatoty Edward, imetwaa mara tano taji la michuano hiyo, 1975 visiwani Zanzibar, 1993 na 1999 mjini Kampala, Uganda na mara mbili mfululizo pia 2011 na 2012 mjini Dar es Salaam.
  Michuano ya Kigali mwaka huu, ilikuwa ni fursa kwao kujaribu kusawazisha rekodi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC waliotwaa mara sita, 1974, 1991 mjini Dar es Salaam, 1992 visiwani Zanzibar, 1995, 1996 mjiji Dar es Salaam na 2002 Zanzibar tena.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BREAKING NEWS; YANGA YAJITOA KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top