• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 31, 2014

  SERIKALI YAJITWISHA ZIARA YA REAL MADRID, DK FENELLA AINGIA ‘MZIGONI’ RASMI

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Maandalizi ya ziara ya kikosi cha magwiji wa Real Madrid ya Hispania, leo imemtembelea Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kumjulisha rasmi juu ya tukio hilo na mwanamama huyo kwa niaba ya Serikali, ameahidi kutoa ushirikiano.
  Kamati hiyo, ambayo wiki iliyopita ilimtembelea 
  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick na kumuelezea rasmi juu ya tukio hilo la mwezi ujao, kwa kiasi kikubwa imepiga hatua ya mafanikio kuelekea ziara hiyo ya kihistoria nchini.
  Waziri Dk Fenella Mukangara wa pili kushoto alipokutana na Kamati ya Maandalizi ya Ziara ya Real Madrid nchini ofisini kwake leo

  Ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Farough Baghozah, Kamati hiyo ilifika ofisi ya Waziri huyo, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ambaye aliwapokea vizuri na kuonyesha kufurahishwa kwa ujumla na jambo hilo.
  Meneja ziara ya magwiji hao wa Real, Dennis Ssebo ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba wamepokewa vizuri na Dk Fenella ambaye amesema Serikali italibeba kwa mikono miwili tukio zima hilo.
  “Tumepokewa vizuri na Mheshimiwa Dk Fenella, na amesema Serikali italibeba hili,”amesema Ssebo uratibu wa ziara hiyo ‘umemkata weiti’ kwa pilika za usiku na mchana, ndani na nje ya nchi. 
  Wachezaji waliotamba kuanzia La Liga, wakacheza ligi nyingine za Ulaya, Kombe la Ulaya, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia waliowahi kuchezea Madrid watakuja nchini Agosti 22.
  Katika ziara hiyo, pamoja na kucheza mchezo wa kirafiki na kikosi maalum cha wachezaji nyota wa Tanzania Agosti 23, pia watafanya utalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo kupanda mlima Kilimanjaro.
  Real Madrid inakuja nchini kwa mwaliko wa kampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Farough Baghozah.
  Miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja na Real nchini ni pamoja na Wanasoka Bora wa zamani wa Dunia, Mfaransa Zinadine Zidane, Mreno Luis Figo na Mbrazil, Ronaldo Lima.
  Magwiji hao wa Real tayari wamekwishafanya matangazo ya ziara yao nchini wakisema wana hamu mno ya kukanyaga ardhi ya Tanzania.
  Kampuni ya Vodacom Tanzania ni miongoni mwa makampuni yaliyojitokeza kudhamini ziara pamoja na Fastjet, Tropical, Pembe Flower, Lake Gas, EFM Radio na Ladger Plaza Bahari Beach.
  Wito umetolewa kwa makampuni zaidi kujitokeza kudhamini ziara hiyo ya kihostoria nchini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERIKALI YAJITWISHA ZIARA YA REAL MADRID, DK FENELLA AINGIA ‘MZIGONI’ RASMI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top