• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 30, 2014

  MUSTAKABALI WA HESHIMA YA MANJI YANGA SC...

  MWISHONI mwa wiki, klabu ya Yanga SC ilitangaza Kamati mpya ya Utendaji kufuatia ridhaa aliyopewa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji katika mkutano na wanachama baada ya kumaliza muda wake.
  Yanga SC ilistahili kuingia katika uchaguzi mpya mwezi huu, lakini Manji akaomba ridhaa ya wanachama kukaa kwa mwaka mmoja zaidi yeye na makamu wake, Clement Sanga ndipo aitishe uchaguzi mpya.  
  Manji aliomba ridhaa ya kuunda Kamati mpya ya Utendaji atakayofanya nayo kazi katika kipindi hicho kingine, ambayo alipewa.

  Na baada ya ridhaa hiyo, akateuwa Kamati mpya ya Utendaji inayoundwa na Wajumbe Abubakar Rajabu atakayesimamia pia Mradi wa Jangwani City, Sam Mapande atakayesimamia pia Sheria na Utawala Bora, George Fumbuka atakayesimamia pia Uundwaji wa Shirika.
  Wengine ni Waziri Barnabas atakayesimamia pia Vibali vya Hatimiliki na Mahusiano na Wafadhili, Abbas Tarimba atakayesimamia pia Mipango na Uratibu, Isaac Chanji na Seif Ahmed ‘Magari’ watakaosimamia pia Uendelezaji wa Mchezo, Mussa Katabalo atakayesimamia pia Mauzo ya Bidhaa. Mohammed Bhinda atasimamia pia Ustawishaji wa Matawi, David Ndeketela Sekione atasimamia pia Uongezaji wa Wanachama, Mohammed Nyenge atasimamia pia Utangazaji wa Habari, Taarifa na Matangazo.
  Wajumbe hao, pia wataongoza Kamati ndogo ndogo, Mapande Kamati ya Maadili, Nidhamu na Uchaguzi, Fumbuka na Barnabas Kamati ya Uchumi na Fedha, Chanji na Magari Kamati za Ufundi, Mashindano na Soka ya Vijana na Wanawake.
  Wajumbe waliotemwa ni pamoja Abdallah Bin Kleb, Salum Rupia, George Manyama, Aaron Nyanda na Lameck Nyambaya. 
  Manji aliingia madarakani Julai mwaka juzi, katika uchaguzi mdogo kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga, Makamu wake Davis Mosha na Wajumbe kadhaa, ambao kwa pamoja walikuwa wamebakiza miaka miwili madarakani.
  Maana yake- Manji na Kamati yake mpya ya Utendaji walitakiwa kuitisha uchaguzi mwingine baada ya kumalizia muda wa akina Nchunga- lakini wakaomba mwaka mmoja zaidi.
  Wakati Manji anaingia madarakani miaka miwili iliyopita, wana Yanga walikuwa wana matumaini makubwa ya kuona mabadiliko makubwa katika klabu yao.
  Hiyo ilitokana na ahadi zake mwenyewe Manji- kwamba angejenga uwanja wa kisasa na kwa ujumla kuifanya klabu ijitegemee na kujiendesha kisasa.
  Katika siku za mwanzoni, Manji alionyesha kuwa na dhamira ya kweli ya kutekeleza hayo, baada ya kuunda Kamati mbalimbali, ikiwemo ya kuendeleza jengo dogo la klabu hiyo liliopo Mtaa wa Mafia na ya ujenzi wa Uwanja, uliopewa jina mradi wa Jangwani City.
  Hata hivyo, siku zimeenda na hadi amemaliza kipindi chake cha kwanza stahili cha kuongoza klabu- na hakuna alichotekeleza. Yanga bado ni ile ile kama alivyoikuta.
  Hii maana yake, Manji amewangusha wana Yanga waliomuamini hata wakamuunga mkono na kumpigia kura awe kiongozi wao mkuu.
  Lakini kitendo cha kuomba mwaka mmoja zaidi maana yake anajua alijikwaa wapi na sasa anataka kuwafurahisha wana Yanga.
  Na kitendo cha kuunda Kamati mpya ya Utendaji, labda alikwamishwa na baadhi ya watu aliokuwa nao katika kipindi cha awali, sasa ameachana nao na kuunda timu mpya ya mafanikio.
  Siku hazigandi. Mwaka mmoja utaisha na wakati utatoa majibu, Manji amefanya nini Yanga SC.
  Hivyo basi, Manji anatakiwa kujua mustakabali wa heshima yake ndani ya Yanga na mbele ya wana Yanga kwa ujumla upo ndani ya mwaka mmoja aliouomba. Eid Mubarak. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MUSTAKABALI WA HESHIMA YA MANJI YANGA SC... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top