• HABARI MPYA

    Monday, July 21, 2014

    NOOIJ: BADO TUNA NAFASI YA KUSONGA MBELE AFCON

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Tanzania, Taifa Stars amesema anaamini bado ana nafasi ya kuitoa Msumbiji kwenye hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco, licha ya kulazimishwa sare ya 2-2 jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mchezo wa jana, Mholanzi huyo alisema kwamba timu yake imekuwa ikipata mabao katika kila mechi, chini yake na ana matumaini hali hiyo itaendelea hata katika mchezo wa marudiano na Mambas.
    Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij bado ana matumaini ya AFCON 2015

    “Tulipata ushindi mwembamba dhidi ya Zimbabwe nyumbani (1-0), lakini tukaweza kwenda kupata mabao mawili Harare na kutoa sare ya 2-2 tukafuzu, naamini hata Maputo tunaweza kufunga,”alisema Nooij.
    Akiuzungumzia mchezo huo, Nooij alisema alijua mapema utakuwa mgumu na pamoja na kutengeneza nafasi nyingi, lakini walipata mabao mawili- ingawa makosa ya safu yake ya ulinzi yaliwapa pia mabao Msumbiji.
    “Walitangulia kupata bao, refa alitoa penalti, hao ndiyo marefa huwezi kusema kitu, tukafanikiwa kusawazisha na kupata bao la pili, lakini bahati mbaya wakasawazisha. Tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wa marudiano. Tutafanyia kazi makosa na kwenda kupigana tuweze kufuzu, nafasi bado tunayo,”alisema.  
    Mabao ya Stars jana yalifungwa na kiungo wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa. 
    Dakika 45 za kwanza zilimalizika bila bao na kipindi cha pili, Msumbiji walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 47 kwa penalti iliyokwamishwa nyavuni na Elias Pelembe baada ya Kevin Yondan kumcheza rafu kwenye eneo la hatari. Mcha aliisawazishia Stars bao hilo dakika ya 65 akimalizia krosi nzuri ya Thomas Ulimwengu.
    Mcha tena akaifungia Stars bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 71 kwa penalti, baada ya mabeki wa Mambas kumchezea rafu Mbwana Samatta kwenye eneo la hatari.
    Stars iliongeza mashambulizi langoni mwa Msumbiji na kukosa mabao kadhaa ya wazi. Msumbiji walizinduka na kufanya shambulizi zuri lililowapatia bao la kusawazisha dakika ya 87 kupitia kwa Isaac Carvalho aliyetokea benchi pia.
    Stars sasa itajitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele, au sare ya kuanzia mabao 3-3, wakati wenyeji wanaweza kunufaika na sare ya 1-1 au 0-0. Ikiwa 2-2 tena, mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
    Stars iliyofika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 1-0 nyumbani na sare ya 2-2 Harare, ikifanikiwa kuitoa Msumbiji itapangwa katika Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya Morocco mwakani. 
    Stars imekuwa ikinyanyaswa na Msumbiji miaka ya karibuni na mara mbili imewahi kutolewa na Mambas katika hatua za awali za AFCON. Kuwania Fainali za Ghana mwaka 2008, Stars ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ilifungwa 1-0 Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa kundi.
    Kuwania Fainali za mwaka jana Afrika Kusini, Stars ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen, ilitolewa kwa penalti 5-4 na Msumbiji baada ya sare ya jumla ya 2-2. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NOOIJ: BADO TUNA NAFASI YA KUSONGA MBELE AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top